YANGA HAIKAMATIKI, YALIPA KISASI KWA KAGERA




Mshambuliaji wa Yanga Said Bahanuz, akijaribu kumfunga kipa wa Kagera Sugar Hannington wakati wa mechi ya Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.Picha na Jackson Odoyo

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga jioni ya leo imeendelea kutakata kileleni kwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar.
Bao hilo pekee lilitupiwa kambani na kiungo wa kimataifa Haruna Niyonzima 'Fabregas', na kuiwezesha Yanga kulipa kisasi kwa Kagera waliowatungua kama hivyo katika mechi yao ya kwanza iliyochezwa Oktoba 8 mwaka jana mjini Kagera.
Niyonzima alifunga bao hilo dakika ya 66 ya mchezo huo likiwa bao lake la pili mfululizo katika ligi kufuatia Jumamosi alipatia Yanga ushindi kama huo mbele ya Azam.
Katika mechi hiyo Yanga ilikosa penati katika kipindi cha kwanza baada ya Didier Kavumbagu kushindwa kufunga mkwaju wa adhabu hiyo iliyolewa na mwamuzi baada ya yeye mwenyewe kuchezewa faulo.
Kwa ushindi wa leo ambao umezima tambo za Kagera walioapa ni lazima waizamishe tena Yanga, imeifanya vinara hao kufikisha pointi 42 kutokana na mechi 18, ikiiacha Azam yenye pointi 36.
Katika mechi nyingine zilizochezwa leo, Coastal Union ya Tanga ikiwa nyumbani uwanja wa Mkwakwani ililazimishwa suluhu na Ruvu Shooting na kufikisha pointi 31 sawa na Simba japo inaendelea kusalia nafasi ya nne.
Wababe wa Simba, Mtibwa Sugar wakiwa uwanja wao wa Manungu ilijikuta ikilazimisha sare ya bila kufungana na maafande wa Prisons Mbeya, huku Polisi Moro iliendelea kuimarika kwa kuinyuka maafande wenzao wa Mgambo JKT ya Muheza Tanga kwa bao 1-0.
Bao hilo pekee la Polisi inayonolewa na nyota w zamani wa Pan na Yanga, Mohammed Rishard 'Adolph' Ally Jangalu lililowekwa kimiani na Kondo Salum kwa mkwaju wa penati katika kipindi cha pili.
Pambano jingine lililokuw alichezwe leo kati ya wenyeji JKT Ruvu dhidi ya Toto African, mechi hiyo imeahirishwa hadi kesho kutokana na kupisha pambano la Yanga na Kagera lililochezwa taifa.
Mechi hiyo itachezwa kwenye uwanja wa Chamazi, nje kidogo ya jijini la Dar es Salaam, huku kila kitu ikihitaji ushindi ili kujiweka pazuri katika msimamo wa ligi hiyo inayozidi kushika kasi.

Post a Comment

0 Comments