NGORONGORO vs ZAMBIA 3-3

                           Na Mwandishi Wetu, Gaborone
TIMU ya soka ya vijana chini ya miaka 20 ya Tanzania ilianza kwa kutoka sare ya magoli 3-3 dhidi ya mabingwa watetezi wa mashindano ya COSAFA, Zambia katika mchezo wao wa kwanza wa kundi C uliofanyika kwenye uwanja wa Chuo  Kikuu cha Botswana jijini Hapa.

Yosso wa Tanzania ndio walikuwa wa kwanza kufunga katika mchezo huo katika dakika ya pili kupitia kwa mshambuliaji wake hatari, Simon Msuva.

Zambia ambayo walikuwa wakijiamini sana waliweza kusawazisha mchezo huo katika dakika 13 kupitia kwa Evans Kangwa ambaye aliweza kumpita beki wa Ngorongoro Heroes, Samuel Mkomola.

Msuva aliweza kuiandikia Ngorongoro goli la pili katika dakika 23 lakini Kangwa tena aliisawazishia timu yake dakika tatu baadaye.

Hassan Kessy aliweza kuifungia Ngorongoro goli la tatu kwa kupiga mpira wa kona ulioingia moja kwa moja wavuni na kuifanya Tanzania imalize kipindi cha kwanza wakiwa mbele kwa magoli 3-2.

Dakika 77 Alex Sichone alifuta ndoto za yosso wa Tanzania kumaliza wakiwa kidedea baada ya kuisawazishia timu yake goli hilo la tatu.

Timu hiyo tegemeo kwa Tanzania ilikosa pia penati katika dakika ya 44 kupitia Msuva huku Zambia walioamka katika kipindi cha lala salama mashambulizi yao yaliokolewa na mabeki wa Ngorongoro Heroes.

Wakati huo huo, Yosso wa Afrika Kusini ambao pia wako kundi C walianza vyema mashindano hayo kwa kuifunga Mauritius magoli 4-0 na hivyo ndio wanaongoza katika kundi hilo.

Ngorongor Heroes itashuka tena dimbani Jumapili kucheza na Afrika Kusini kwenye uwanja wa Molepolole kuanzia saa 11 saa za Tanzania.

Post a Comment

0 Comments