TTCL YASAIDIA VITUO VYA WATOTO SIKUKUU YA EID




Mkuu wa Masoko na Mauzo wa kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL), Bw.Peter Ngota akikabidhi msaada wa vyakula kwa Mwenyekiti wa Shirika la Femele Youth Help Age Trust,Bw Simon Mganga lililoko Pangani-Kibaha linalohudumia watoto yatima,na wanaoishi katika mazingira magumu katika hafla iliyofanyika jijini Dar es salaam jana kusherehekea sikukuu ya Eid.
Mkuu wa Masoko na Mauzo wa kampuni ya Mawasiliano Tanzania, Bw.Peter Ngota akikabidhi msaada wa vyakula kwa wawakilishi wa shirika la Missionary of Charity la watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu katika hafla iliyofanyika jijini Dar es salaam jana kusherehekea sikukuu ya Eid.

Na mwandishi wetu, Dar es salaam

Wadau wa maendeleo wametakiwa kuendeleza juhudi za kusaidia jamii hasa watu waishio katika mazingira magumu ili kuleta maendeleo na ustawi katika jamii.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Masoko na Mauzo wa kampuni ya Mawasiliano Tanzania, Bw.Peter Ngota jijini Dar es salaam jana wakati akikabidhi msaada wa vyakula kwa vikundi vya watu wenye mahitaji ikiwa ni sehemu ya kampuni hiyo kushiriki katika kusaidia jamii na kusherehekea sikukuu ya Eid.

Akizungumza katika hafla hiyo alisema kuwa kuna umuhimu wa wadau mbalimbali kushiriki katika kusaidia makundi ya watu wenye mahitaji ili nao waweze kupata huduma za msingi ikwemo elimu, afya na chakula.

Amesema kuwa TTCL inatambua uwepo wa makundi hayo ndio maana imeamua kuungana nao hasa wakati huu wa sikukuu ya eid el fitri ili nao watambue kuwa wanathaminiwa kama sehemu ya jamii.

Bw. Ngota amesema kuwa kampuni hiyo imekuwa ikishiriki katika shughuli za kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kusaidia jamii katika sekta mbalimbali.

Kwa upande mwingine, aliwaasa watoto wanaosaidiwa na vituo hivyo kujitahidi katika masomo na kufanya vizuri ili waje kufanya kazi katika kampuni hiyo ya wazawa hapa nchini.

“Nawaasa mjitahidi katika masomo ili hapo baadaye mje kufanya kazi katika kampuni hii,” alisema. Akizungumza kwa niaba ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu,mtoto Emiliam Joseph ameishukuru kampuni hiyo kwa msaada huo na kuomba wadau wengine kuendeleza juhudi hizo.

Mwenyekiti wa shirika linalohudumia watoto yatima na wanaoishi katika mazigira magumu,Femele Youth Help Age Trust, Bw. Simon Mganga ameishukuru kampuni hiyo kwa msaada huo na kukiri kuwa kampuni hiyo imekuwa mmoja wa wadau muhimu katika kusaidi shirika lake.

Naye mwakilishi wa shirika la Missionary of Charity, St Mary Domitila amesemakuwa msaada waliopata una thamani kubwa kwao kwani itoaji wa msaada huwa hauangalii kiasi bali ni nia ya dhati ya mtu kuamua kusaidia na hivyo kutoa wito kwa wadau wengine keundelea kusaidia.

Msaada huo wenye jumla ya Tsh milioni tatu unajumuisha mchele,unga wa mahindi,mafuta ya kupikia na majani ya chai.
Pia TTCL ilitoa simu kwa mashirika hayo katika juhudi za kuwarahisishia mawasiliano.

Kwa muda mrefu sasa, TTCL imekuwa ikishiriki kutoa msaada kwa vituo vinavyohudumia watu wanaoishi katika mazingira magumu.

Post a Comment

0 Comments