Uncle JJ (kushoto) na Uncle D anayejaribu kuvaa viatu vyake |
Uncle D |
BADO mashabiki wa filamu nchini wanaendelea kuumizwa na kifo cha
aliyekuwa nyota wa fani hiyo, Steven Kanumba 'Uncle JJ' ama lile maarufu
la 'The Great Pioneer' aliyefariki ghafla Aprili mwaka huu.
Tangu
alipofariki dunia, mashabiki wake wamekuwa wakisikilizia na kutaka kuona
nani atakayeweza kuvaa viatu vya mkali huyo aliyekuwa na kiu kubwa ya
maendeleo katika fani yake tangu alipokuwa Kaole Sanaa.
Wengi
wamekuwa wakijiuliza ni msanii gani atakayeweza kuwaburudisha kwa
kiwango alichokuwa akikifanya Kanumba hasa kupitia filamu zake
mchanganyiko zikiwemo za kiutu uzima, watoto, kidini na masuala mengi ya
kijamii.
Japo wapo wasanii kibao waliowahi kufanya kazi pamoja na
Kanumba wamekuwa wakiaminiwa huenda wakasimama na kuziba pengo hilo la
msanii huyo, hata hivyo hali inaonekana kuwa ngumu.
Hii inatokana na
ukweli kwamba marehemu Kanumba, aliiteka mioyo ya mashabiki wengi kiasi
imekuwa vigumu kwa mashabiki hao kuruhusu mioyo hiyo kutoa nafasi kwa
mtu mwingine kuingia.
Ndio maana hata soko la filamu lilionekana
kuyumba tangu Kanumba alipofariki kwa kazi za watu wengine kusahauliwa
kwa muda na kukimbiliwa kazi za nyuma za mkali huyo, ingawa kwa sasa
hali inaendelea kubadilika kwa watu kuzoea hali halisi iliyotokea.
Hata
hivyo, huenda mashabiki wa filamu wakasuuzwa roho zao, baada ya
Jacklyne Wolper kuamua kutengeneza filamu mpya iitwayo 'After Death'
ambayo imemshirikisha msanii asiye na jina, lakini aliyeshabihiana na
marehemu Kanumba.
Msanii huyo si mwingine bali ni Philemon Latwaza ambaye ndani ya filamu hiyo mpya atafahamika kwa jina la 'Uncle D'.
Uncle
D, ameigiza na 'watoto wa Kanumba', Jennifer na Patrick, walioibuliwa
na filamu za 'Uncle JJ' na 'This is It', sambamba na waigizaji wengine
wenye majina waliowahi kucheza pamoja na marehemu Kanumba enzi za uhai
wake.
Muongozaji wa filamu hiyo, Leah Richard Mwendamseke 'Lamata'
alisema ujio wa Uncle D unaweza kuziba pengo la Kanumba kwa kiasi fulani
na pengine kuwarudisha mashabiki wa marehemu huko katika 'sononi' mpya
ya kumkumbuka.
Lamata, alisema wamefyatua filamu hiyo kama njia ya
kumuenzi Kanumba na pia kuendelezaa juhudi zake za kuibua na kukuza
vipaji vya akina Jennier na Patrick.
"Nadhani After Death,
itawakumbusha mbali mashabiki wa filamu kwa namna Uncle D alivyomudu
kumuigiza Kanumba na hasa kutokana na kufanana naye kwa sura kwa kiasi
kikubwa," alisema.
Mbali na Uncle D na watoto Jennifer na Patrick
katika filamu hiyo pia wameigiza akina Mainda, Mayasa Mrisho, Ben
Blanco, Wolper mwenyewe, Irene Paul, Shamsa Ford na Patcho Mwamba.
Swali
la kujiuliza je, Uncle D atamudu kuvaa viatu vya Kanumba kama Lamata
anavyodai? Ni suala la kusubiri kuona mara filamu hiyo itakapoachiwa
mtaani.
0 Comments