Social Icons

Thursday, May 21, 2015

MSAMA ATENGANISHA WAIMBAJI WA INJILI NA SIASA


MKURUGENZI wa Kampuni ya Msama Promotions ambayo ndio inaandaa matamasha ya Pasaka na Krismasi, Alex Msama amekemea waimbaji wa muziki wa injili Tanzania akiwataka  kufanya kazi ya Mungu na kuachana na siasa ambazo zinawaondoa kwenye uinjilisti.
Msama ameyasema hayo wakati tukielekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Madiwani, Wabunge na urais unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Msama anasema karipio hilo linawahusu pia viongozi wa dini wakiwamo wachungaji na maaskofu  ambao wanaonyesha nia ya kutaka kuwania uongozi wa kisiasa katika nafasi hizo tatu.
Sababu za Msama kukemea waimbaji wa injili kujihusisha na wanasiasa wakiwamo wagombea urais, kuna baadhi ya waimbaji wametunga nyimbo za ‘kuwatukuza’ wagombea urais wakati wao wanatakiwa muda wote kumtukuza Mungu na si binadamu wenzao.
“Waimbaji tunatoka katika mstari, kwani Mungu anawategemea kufikisha ujumbe wake kwa lengo la kuachana na machukizo ambayo yanapoteza mwelekeo wa jamii mbalimbali ambazo zinahitaji maono ya Wainjilisti,” alisema Msama na kuongeza:
“Waimbaji ambao ninashirikiana nao katika kufikisha huduma ya neno la Mungu, nashangaa wanatoka katika mstari, nawaomba wamrudie Mungu kwani wanapotea wakiwatumikia mabwana wengine.” 
Alisema kitendo wanachokifanya waimbaji na wachungaji ni kinyume na huduma ndani ya mioyo yao kwa sababu wanachokifanya si sahihi.
Anafafanua kwamba kazi ya muziki wa injili ni kuhubirisha, waimbaji ni wainjilisti wanawatoa waovu kwa shetani na kuwapeleka kwa Mungu ambaye ndiye tegemezi kwa binadamu wote.
“Ni jambo la kusikitisha sana, wanamhuzunisha Bwana Yesu, alipoondoka kwenda mbinguni aliwaambia wafuasi wake,  nendeni ulimwenguni kote mkaihubiri injili yangu, mwenye kuamini ataokoka na asiyeamini ameangamia,” alieleza Msama.
Anasema kwa kufanya hivyo waimbaji hao ndio wanahubiri uovu kwa kuwapamba wachafu  na kuwafananisha na Yuda Eskariot aliyemsaliti Yesu  kwa ajili ya pesa na kuwataka waliofanya hivyo waache mara moja.
Msama anaendelea kueleza na kufafanua kupitia maandiko matakatifu  kwamba ya Kaisari wamwachie Kaisari, mwenye kupewa sifa na wao ni Mungu peke yake, mwanadamu hawezi kupewa sifa na kuinuliwa kwa sifa.
Pia anawakemea wagombea urais waache kuwatumia waimbaji  wa injili na kujificha kwenye kanisa kwamba ndio sehemu ya kuombea kura na kugawa pesa makanisani, Mungu hahongwi na waache pia kumchokoza Mungu kwani akichukia zaidi mwisho wake ni mbaya.
Anasema siasa na dini ni vitu viwili tofauti kwani kwenye siasa uongo ni mwingi ambao katika uinjilisti hautakiwi kwa sababu unakwenda tofauti na maandiko matakatifu ya Mungu.
“Nahuzunishwa na wanaotumia mfumo huo kwa sababu siasa inayohubiriwa ni ya kumjenga mgombea urais na kumpamba, wakati katika maandiko matakatifu hakuna mambo ya kupambana kama inavyofanyika sasa,” alisema.
Anaeleza kwamba wachungaji wanasahau kazi zao ambazo ni kuwachunga kondoo wa Mungu  na kuhubiri injili na si lingine lolote.
“Nia zao wakazitangaze huko na wakiendelea nitawaweka hadharani kwani nitawaumbua kwa kuwaeleza kwamba hawafai kuwa marais kwa mtindo wanaoutumia,” alisema.
Msama ndiye ‘anayedili’ na waimbaji wa muziki wa injili waache na watubu sambamba na kukiri makosa yao kwa Mungu na waachane na dhambi ambayo ni kero kwa Mungu.
Wachungaji wanaojielekeza kwenye siasa waache mpangilio huo kwa sababu haiwezekani kuwatumikia mabwana wawili na kazi yao kwa Mungu ni injili pekee.

“Ukijikita huko utakuwa huna muda wa kumtumikia Mungu, siasa inasababisha kusema uongo wakati uchungaji una heshima kubwa,” alisema Msama.

No comments:

 
 
Blogger Templates