Social Icons

Thursday, July 26, 2012

TFF, BENKI ZASAINI UDHAMINI WA BancABC SUPER 8

Benki ya ABC imesaini mkataba wa miaka mitatu na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kudhamini michuano ya BancABC Super 8 inayoshirikisha timu nane, nne kutoka Tanzania Bara na nyingine nne kutoka Zanzibar.

Hafla ya utiaji saini imefanyika leo (Julai 26 mwaka huu) kwenye ofisi za TFF, Dar es Salaam ambapo Katibu Mkuu Angetile Osiah amesaini kwa niaba ya shirikisho wakati kwa upande wa ABC, saini yake iliwekwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo kwa Tanzania, Boniface Nyoni.

Mashindano hayo yataanza Agosti 4-18 mwaka huu yakichezwa katika miji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Zanzibar ambapo timu zote shiriki zitacheza katika vituo hivyo.

Uzinduzi rasmi wa mashindano hayo utafanywa Agosti 2 mwaka huu na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa benki ya ABC yenye makao yake makuu nchini Botswana, na ina matawi katika nchi za Msumbiji, Zambia, Tanzania, Zimbabwe.

Katika uzinduzi huo, CEO ataelezea thamani ya mkataba huo ambapo utahusisha gharama za malazi, usafiri, vifaa na uendeshaji wa mashindano hayo.

Akizungumza baada ya kutia saini, Osiah amesema hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya TFF kuwa na mashindano mengi yatakayosaidia kuziandaa timu kabla ya kuanza Ligi Kuu.

Naye Nyoni amesema ABC imekubali kuingia kudhamini mpira wa miguu ikiwa ni lengo la kuchangia ustawi wa mchezo huo na kutoa sehemu ya faida wanayopata kwa kupitia michezo.

Timu zitakazoshiriki mashindano hayo ni zile zilizoshika nafasi tatu za juu katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara na Ligi Kuu ya Zanzibar. Nyingine ni timu iliyoshika nafasi ya kwanza kwenye Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara na Ligi Daraja la Kwanza ya Zanzibar ambazo nazo kwa kushika nafasi hizo zimeshaingia katika Ligi Kuu.

RAMBIRAMBI MSIBA WA MCHEZAJI ISSA KIHANGE
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa zamani wa timu ya Simba, Issa Kihange kilichotokea juzi (Julai 24 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti akiwa mchezaji Kihange alitoa mchango mkubwa kwa timu mbalimbali alizochezeaz ikiwemo Simba na CDA ya Dodoma, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Kihange, klabu za Simba na CDA na na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Mungu aiweke roho ya marehemu Kihange mahali pema peponi. Amina

HATIMAYE FLYING EAGLES YATUA KUIVAA NGORONGORO HEROES
Hatimaye timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Nigeria (Flying Eagles) imewasili nchini leo mchana (Julai 26 mwaka huu) kwa ndege ya RwandAir ikiwa na msafara wa watu 32 wakiwemo wachezaji 18.

Awali timu hiyo ilikuwa iwasili jana jioni (Julai 25 mwaka huu) ikitokea Kigali, Rwanda lakini ikashindwa baada ya kuchelewa ndege. Flying Eagles itapambana na Ngorongoro Heroes katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili itakayofanyika Jumapili (Julai 29 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.

Mechi hiyo ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za 18 za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 zitakazochezwa mwakani nchini Algeria itachezeshwa na waamuzi kutoka Kenya wakati Kamishna ni Charles Masembe kutoka Uganda.

Flying Eagles ambayo iko chini ya kocha John Obuh, Julai 24 mwaka huu ilicheza mechi ya kirafiki na Rwanda (Young Amavubi) kwenye Uwanja wa Amahoro jijini Kigali na kufungwa bao 1-0.

Msafara wa timu hiyo unaongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Nigeria (NFF), Chris Green umefikia hoteli ya Rungwe iliyoko Mtaa wa Livingstone, maeneo ya Kariakoo.
Baadhi ya wachezaji walioko katika kikosi cha Flying Eagles ni Chidi Osuchukwu, Alhaji Gero, Shehu Abdullahi, Aminu Umar, Aliyu Mohamed, Uche Agbo, Jonah Usman, Harrison Egbune, Hassan Abubakar na Yahya Adamu.

Makocha wote, Jakob Michelsen wa Ngorongoro Heroes na Obuh wa Flying Eagles wakiwa na manahodha wao, Jumamosi (Julai 28 mwaka huu) saa 4 asubuhi watazungumza na waandishi wa habari juu ya walivyoviandaa vikosi vyao kwa ajili ya mechi hiyo. Mkutano huo utafanyika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 3,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani wakati VIP B na C itakuwa sh. 5,000. Kiingilio kwa VIP A itakuwa sh. 10,000.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

 
 
Blogger Templates