Social Icons

Wednesday, August 18, 2010

Yanga waifunga Simba pambano la Ngao ya Hisani

TIMU ya Yanga jana ilifanikiwa kutwaa Ngao ya Jamii baada ya kuwafunga watani wao Simba mabao 3-1, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.Mshindi wa mechi hiyo alipatikana kwa mikwaju ya penalty baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 bila kufungana.
Ushindi huo kwa Yanga, ni kama kulipa kisasi cha Aprili 18 ambapo ilifungwa mabao 4-3 katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu ya Bara.Katika upigaji wa penalty, Simba walikuwa wa kwanza, lakini Emmanuel Okwi alikosa.Hapo ikawa zamu ya Yanga ambapo Ernest Boakye alipiga na kukosa, lakini mwamuzi Ramadhan Ibada akaamuru arudie na ndipo akapata.Baada ya hapo, ikawa zamu tena ya Simba, Uhuru Selemani akakosa kabla ya Godfrey Bonny naye kukosa.
Baada ya hapo, ikawa zamu ya Simba tena kupiga penati ya tatu ambayo hata hivyo, Amri Kiemba nayo akakosa penati ya tatu mfululizo.Penalti ya tatu kwa Yanga ilikwenda kupigwa na beki wake wa kushoto, Stefano Mwasika ambaye alifanikiwa kumtungua kipa Ally Mustapher ‘Barthez.’Mkwaju wa nne kwa Simba, ulipigwa na Mohamed Banka ambaye alipata, hivyo macho ya maelfu ya mashabiki yakaelekea kwa Isaack Boakye wa Yanga.Kitendo cha sentahafu huyo wa kimataifa wa Ghana, kupata penalty hiyo, ikawa mwisho wa mechi hiyo kwani, tayari Yanga walikuwa mbele kwa mikwaju 3-1. Ni mara ya kwanza Yanga kushinda kwa mikwaju ya penalty.
Kwa ushindi huo, Yanga iliyo chini ya Kocha Kostadin Papic, itaanza kampeni ya Ligi Kuu hapo Agosti 21 kwa furaha ya kumfunga mtani wake.Aidha, ushindi huo ni faraja kubwa kwa uongozi mpya wa Yanga chini ya Mwenyekiti wake Lloyd Nchunga ulioingia madarakani Julai 18.
Wakati Nchunga na kamati yake wakiwa kwenye faraja, uongozi mpya wa Simba ambao uliingia madarakani Aprili 9 chini ya Mwenyekiti wake Ismail Aden Rage, ni maumivu.
Simba itaanza kampeni ya Ligi Kuu dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Uhuru huku Yanga akianza na Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.Ndani ya dakika 90, Yanga walikuwa wa kwaza kufanya shambulizi la nguvu langoni mwa Simba katika dakika ya tano baada ya Nsa Job kumlamba chenga Joseph Owino, krosi yake ilitolewa. Dakika ya 14, Yanga walifanya shambulizi tena kwa Nsa Job kugongeana vizuri na Abdi Kassim ‘Babi,’ lakini umaliziaji ukawa mbaya.Dakika moja baadaye, Simba walijibu shambulizi hilo kwa Mussa Hassan Mgosi kuichambua ngome ya Yanga, lakini shuti yake ikienda nje.Timu hizo ziliendelea kucheza soka ya kuvutia na kushambuliana kwa nguvu na katika dakika ya 22, Okwi alipata nafasi nzuri ya kuweza kufunga, alikosa.Licha ya Okwi kuwalamba chenga mabeki wa Yanga, Uhuru Selemani alipiga shuti hafifu mithiri ya beki anayerudisha mpira kwa kipa wake.Dakika ya 26, Isack Boakye wa Yanga, alilimwa kadi ya njano kwa mchezo mabaya dhidi ya Jerry Santo, nyota wa kimataifa wa Kenya.Dakika ya 38, Mgosi alilimwa kadi ya njano baada ya kuonyesha jazba dhidi ya maamuzi ya mwamuzi baada ya kumchezea vibaya Boakye wa Yanga. Katika dakika ya 43, Santo alilimwa kadi ya njano kwa kumchezea vibaya Stefano Mwasika.Hadi timu hizo zinakwenda mapumziko, hakuna timu iliyokuwa imepata bao, licha ya kuwepo kwa kosa kosa nyingi kwa milango yote.Kipindi cha pili, Simba iliyo chini ya Kocha Mzambia, Patrick Phiri akisaidiwa na Syllersaid Mziray, Selemani Matola na Amri Said ‘Stam’, alimtoa Santo na kuingia Amri Kiemba.Naye Mserbia wa Yanga, Kostadin Papic alimtoa Asamoah na kuingia Jerry Tegete.Dakika ya 72, Job alipata pasi nzuri kutoka kwa Tegete, alishindwa kufunga na dakika ya 81, Uhuru alimchezea vibaya Mwasika, hakuna kadi ambayo ilitolewa.
Hadi mwamuzi Ibada anamaliza dakika 90, kulikuwa hakuna bao, hivyo kuingia hatua ya mikwaju ya penalty.Akizungumzia mechi hiyo, Kocha Phiri wa Simba, alisema wao walikuwa washinde ndani ya dakika 90, lakini mwamuzi aliwanyima mikwaju miwili ya penalty.
Naye kocha wa Yanga, Papic alisema vijana wake wamedhihirisha ubora wao na kuhusu Keneth Asamoah, alisema naye amecheza vizuri. Simba: Ally Mustapher ‘Barthez,’ Haruna Shamte, Juma Jabu, Juma Nyosso, Joseph Owino, Jerry Santo/Amri Kiemba, Nico Nyagawa/ Shija Mkina, Mohamed Banka, Mussa Hassan Mgosi/ Patrick Ochan, Emmanuel Okwi na Uhuru Selemani.Yanga: Yaw Berko, Shadrack Nsajigwa/ Fred Mbuna, Stefano Mwasika, Nadir Haroub ‘Cannavaro,’ Isaack Boakye, Nurdin Bakari, Athumani Idd ‘Chuji/ Godfrey Bonny,’ Keneth Asamoah/Jerry Tegete, Nsa Job na Abdi Kassim ‘Babi’/ Yahya Tumbo.
Baadhi ya mashabiki wa Yanga wakishangilia.
Kocha wa Simba Patrick Phiri mara baada ya matokeo hapa akizungumza na wanahabari.
Mashabiki wa Yanga wakishangilia mkwaju wa kwanza ulipoingia.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga Davis Mosha akishika Ngao na wachezaji wa Yanga mara baada ya ushindi.
Kikosi cha Simba kikiomba dua.
Kocha wa Yanga Costadic Papic akitoa maelekezo kwa vijana wake kabla ya kuanza kupiga mikwaju iliyowalaza watani wao Simba.

No comments:

 
 
Blogger Templates