Mfalme Carl XVI Gustaf wa Sweden, amemuaga aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, katika hafla fupi iliyofanyika kwenye Jumba la Kifalme jijini Stockholm, leo tarehe 19 Machi, 2026.
Katika mazungumzo yao mafupi, viongozi hao walijadiliana namna ya kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili katika sekta za nishati, mazingira, kilimo, utalii, miundombinu, madini na teknolojia.
Mfalme Gustaf aliipongeza Tanzania kwa kuweka utulivu nchini na kubuni mipango thabiti ya kutafuta maendeleo na kukuza uchumi wake licha ya changamoto nyingi zinazoikabili dunia nzima hivi sasa.
Balozi Matinyi alimshukuru Mfalme Gustaf kwa ushirikiano mzuri alioupata katika kipindi alichohudumu nchini Sweden ambapo Tanzania imefaidika katika sekta za nishati, kilimo, miundombinu, teknolojia na elimu ya juu.
Hii ilikuwa mara ya tatu kwa Balozi Matinyi kukutana na Mfalme Gustaf tangu awasili nchini Sweden mwezi Mei 2025. Mara ya kwanza ilikuwa wakati wa kukabidhi hati zake za utambulisho tarehe 12 Juni, 2025, na tarehe 9 Desemba, 2025, kwenye mazungumzo ya kibalozi ya mwisho wa mwaka.
Imetolewa na Ubalozi wa Tanzania, Stockholm, Sweden,
19 Machi, 2026.

0 Comments