TUTADHIBITI MAKOSA NYAKATI ZOTE BARABARANI PWANI

Mkuu wa Kikosi Cha Usalama Barabarani Mkoa wa Pwani, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Edson Mwakihaba amewataka wamiliki wa vyombo vya moto wanaosafirisha abiria na mizigo  nyakati za usiku kuhakikisha usalama wa vyombo hivyo kabla ya kuingiza vyombo vyao barabarani .

Mwakihaba ameyasema hayo Oktoba 16 akiwa kwenye operesheni maalum ya kukagua makosa   mbalimbali ya usalama barabarani kama ubovu wa magari ikiwemo magari yanayotumia taa moja (chongo), madeni ya serikali na upakiaji mizigo kwa njia ya hatari, viakisi mwanga.
Mwakihaba ameeleza operesheni hii imetokana na uchunguzi uliofanyika na kubaini uwepo wa magari mabovu na yale ambayo madereva wake wamekuwa wakitumia nyakati za usiku kutotii sheria za usalama barabarani na kusabaisha baadhi ya magari  hayo kuharibika hali inayosababisha foleni ambazo siyo za lazima.
"Operesheni hii imeweza kukamata makosa mbalimbali hatarishi na nitoe onyo kwa madereva wanaovunja sheria nyakati za usiku kwamba Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Pwani limejipanga kukabiliana nao ili kuzuia ajali zinazosababishwa na uzembe wao" amesema Mwakihaba.
Naye mmoja wa madereva wa gari ya abiria inaoyofanya safari zake Mbezi kwenda Mlandizi Juma Kassim amelishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kwa kuendesha operesheni hiyo na kueleza kuwa imempa somo kuwa nyakati zote anapaswa kuhakikisha amefanya ukaguzi wa chombo cha moto kabla ya kuingia barabarani ili kuepukana na ajali ambazo zilikua zinazuilika kwa kuheshimu sheria za usalama barabarani.

Post a Comment

0 Comments