TARURA YAUNGANISHA VIJIJI VYA IFINSI, KAMBANGA NA BUGWE WILAYANI TANGANYIKA

Tanganyika, Katavi

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imekamilisha ujenzi wa vivuko na daraja la Mto Mnyamasi lenye urefu wa mita 20 pamoja na kufungua barabara ya Kambanga-Ifinsi yenye urefu wa Kilomita 37 inayounganisha vijiji vya Ifinsi, Kambanga na Bugwe vilivyopo kata ya Tongwe Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi.

Kaimu Meneja wa TARURA Mkoa wa Katavi, Mhandisi Japhet Bengesi ameishukuru serikali kwa kutoa shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja na vivuko na kufungua barabara inayoanzia Kambanga-Ifinsi mpaka Kijiji cha Bugwe ambapo imewezesha wananchi kusafirisha mazao yao kwa urahisi.

“Kikwazo kikubwa kilikuwa katika mto Mnyamasi ambalo ni eneo la bonde hapo awali hakukuwa na mawasiliano lakini kutokana na juhudi za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutuletea fedha, tumeweza kujenga makalavati ya ukubwa tofauti 7 na barabara unganishi ambapo imekuwa mkombozi mkubwa maana hili ni eneo kubwa sana la uzalishaji”, alisema.

Naye, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mnyamasi, Bw. Ngisa Muyanga ametoa pongezi na shukrani kwa serikali kwa kuwatengenezea barabara hiyo ambayo hapo awali ilikuwa haipitiki, wananchi walikuwa wanavuka kwa shida kusafirisha bidhaa zao.

“Tulikuwa tunavuka kwenye maji kipindi cha masika, wakina mama walikuwa wanajifungulia njiani magari yalikuwa hayapiti na tulikuwa tunashindwa kusafirisha biashara zetu, lakini kwa sasa tunaishukuru serikali, watu wanavuka kwa urahisi na magari yanapita katika vipindi vyote”, alisema Bw. Ngisa. 

Wakati huo huo Mkazi wa kijiji cha Ifinsi, Bw. Ibrahimu Temi alisema, kipindi cha nyuma miundombinu ilikuwa tabu walikuwa wanabeba magunia yenye mazao mabegani kuvuka ng’ambo, lakini sasa magari yanaingia kijijini na wanakoboa mpunga na kusafirisha mchele kufikisha Mpanda kwa urahisi.

Kwa upande wake, Bi. Eunice Shola mkazi wa kijiji cha Ifinsi, ametoa shukrani kwa Rais Samia kupata barabara hiyo kwani wanawake walikuwa wanapata shida kuvuka na wengine walijifungulia njiani, sasa hivi hawana shida ya usafiri magari ya wagonjwa yanafika hadi kjijini na kupeleka wananchi hospitali.

Post a Comment

0 Comments