Na Makinikia,Tanga
Jijini Tanga, katika kata ya Usagara karibu na uwanja wa hockey, kuna makaburi ya zamani yenye sehemu ya Kikristo na sehemu nyingine ya kijeshi ya Vita ya Kwanza ya Dunia, ambapo wengi wa waliozikwa ni Wajerumani.
Kati ya makaburi haya, kuna kaburi moja lenye mvuto wa kipekee, likiwa na sanamu ya marumaru nyeupe ya mwanamke aliyejilaza juu ya kaburi hilo. Inasemekana sanamu hiyo inamwonyesha jinsi alivyokutwa akiwa amefariki, akiwa katika hali ya utulivu.
Makinikia yanaonesha kwamba Kaburi hili ni la Alexander Tame, mtoto wa tajiri mmoja wa Kijerumani mwenye asili ya Israeli, Freddie Tame, aliyekuwa akiishi Tanga hadi mwishoni mwa miaka ya 1960.
Maandishi ya Kijerumani kwenye kaburi hilo yanaonyesha kuwa Alexander alizaliwa mwaka 1906 na alifariki dunia mwaka 1929, ikimaanisha kwamba alifariki akiwa na umri wa miaka 23 tu.
Hadithi inayosimuliwa ni kwamba Alexander alikuwa na mchumba wake waliyependana sana na ambaye aliyefariki muda mfupi baada ya kusikia habari za kifo chake.
Kwa upendo na ili kuweka kumbukumbu ya mwanawe na mchumba wake, Freddie Tame alijenga sanamu hiyo nzuri ya marumaru, ikiwa kama ishara ya mapenzi ya vijana hao ambayo hayakutimilika.
Inasemekana pia kuwa sanamu ya Alexander pia ipo juu ya kaburi la mchumba wake huko Ulaya, ikionyesha uhusiano wao wa kimapenzi ambao hata kifo hakikuweza kukatisha.
Mke wa Freddie Tame, Margareth Tame, aliendelea kuishi Tanga, mkabala na uwanja wa Mkwakwani—ambapo sasa ni jengo la TFA—hadi miaka ya 1980, akiwa na kumbukumbu ya mwanawe na mchumba wake wanaokumbukwa milele kupitia sanamu hizo. Sanamu ambazo zinasemekana ndizo zilizoibua usemi wa kwamba "Mapenzi yalizaliwa Tanga.
0 Comments