Afisa Mwandamizi Masuala ya Uchumi katika Ubalozi wa Tanzania nchini Japan Bi. Edna Dioniz Chuku, aliyemwakilisha Balozi Baraka Luvanda katika Hafla ya Uzinduzi wa aina mpya mbili za kahawa ya Tanzania zitakazoanza kuuzwa katika soko la nchi hiyo, akifafanua jambo kwa wageni waliohudhiria hafla hiyo iliyoandaliwa kwa kushirikiana na Kampuni ya ITO EN na TULLY’S COFFEE, tarehe 1 Oktoba 2024.
Kampuni ya ITO EN LTD, kampuni tanzu ya Tully’s Co. Ltd., inayomiliki migahawa maarufu ya Tully’s Coffee, leo, tarehe 1 Oktoba 2024, imezindua aina mbili mpya za kahawa ya Tanzania, nchini Japan. Aina hizo za kahawa ya Tanzania ni BARISTA’S ROAST KILIMANJARO na KIBO TARIME SWEET WASHED, kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.
Uzinduzi huo umeongeza uhakika wa upatikanaji wa kahawa ya Tanzania kupitia migahawa maarufu nchini Japan ya TULLY’S ambapo, mwezi Machi mwaka huu, ITOEN kwa kushirikiana na TULLY’S walizindua kahawa aina tatu za Tanzania, TULLY’s COFFEE BARISTA BLACK KILIMANJARO; TULLY’S COFFEE MY HOME BLACK KILIMANJARO; na TULLY’S COFFEE BARISTA ROAST COLD BREW – KILIMANJARO BLEND, zilizotoka maeneo ya Tarime, mkoani Arusha na mashamba ya GDM yaliyoko Mbozi mkoani Mbeya.
Aidha, uzinduzi huo kumeifanya TULLYS kuongoza kwa uuzaji kwa wingi wa kahawa ya Tanzania unaojumuisha, aina saba za kahawa hiyo, ndani ya miaka miwili zikiwemo, kahawa za GDM FULL WASHED na GDM NATURAL za Mashamba ya GDM mkoani Mbeya, zilizozinduliwa mwezi Agosti, mwaka jana.
IMETOLEWA NA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI JAPAN
TOKYO
Matukio mbalimbali wakati wa Uzinduzi wa Kahawa mbili za Tanzania kupitia Kampuni ya ITO EN na TULLY’S COFFEE, nchini Japan, tarehe 1 Oktoba 2024Hafla ya Uzinduzi huo ilifanyika katika moja ya Migahawa ya TULLY’S uliopo kwenye Stesheni Kuu ya Tokyo ya Reli ya Mwendokasi nchini Japan (JR LINE – TOKYO STATION) ambayo, iliongozwa na Rais wa ITO EN LTD, Bw. Daisuke Honjo pamoja na Rais wa Migahawa ya TULLY’S, Bw. Yoshio Kobayashi; na kuhudhuriwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Japan.
Uzinduzi huo pia ulipambwa na zoezi la uonjaji wa kahawa ya Tanzania lililoshirikisha wataalam wa kahawa (baristas) wapatao 10 wa maeneo mbalimbali nchini Japan; na makampuni mengine makubwa ya kahawa ya Japan ya MARUBENI, MITSUI na ECOM, yenye ubia na Tanzania.
Kampuni ya ITO EN Ltd., ni kampuni inayoongoza kwa biashara ya vinywaji nchini Japan ambayo, ni kampuni tanzu ya Tully’s Coffee inayomiliki migahawa ya kahawa takriban 700 nchini Japan na imejipatia umaarufu mkubwa katika biashara ya uuzaji wa kahawa za aina mbalimbali duniani.
Kuzinduliwa kwa aina nyingine mbili mpya za kahawa nchini Japan, kunaendelea kupandisha zaidi uhakika wa soko la kahawa ya Tanzania, Japan ambayo imejizolea umaarufu mkubwa kwa ubora na radha ya aina yake na kupelekea kupewa jina maarufu la kibiashara la Kilimanjaro Coffee. Kilimanjrao Coffee ni miongoni mwa brand tatu duniani zinazopendwa zaidi Japan; na jina hilo hutumika nchini humo kwa kahawa zinazozalishwa Tanzania pekee, kwa kutambua kivutio kikubwa cha Mlima Kilimanjaro uliopo nchini Tanzania.
Kwa sasa, Tanzania inauza kahawa yake Japan kwa wastani wa asilimia 34 ya kahawa inayolimwa nchini kutoka asilimia 32 ya mwaka jana, ambayo ni sawa na wastani wa kilogramu million 15 (tani 15,000) ya kahawa yote ya Tanzania inayouzwa nchini Japan. Takwimu hizo zinaendelea kuiweka Japan kuwa mnunuzi mkubwa na namba moja (1) wa kahawa inayolimwa nchini.
0 Comments