Social Icons

Sunday, April 5, 2015

MALKIA POSA YA BOLINGO KUPAMBA USIKU WA MASAUTI

MWANAMUZIKI nyota wa kike anayetamba na kibao kinacho lalama kuhusu mapenzi, ‘Posa ya Bolingo’ Alicious Theluji pichani juu, anatarajiwa kupamba onyesho la ‘Usiku wa Masauti’ litakalofanyika jijini Dar es Salaam, Aprili 18 mwaka huu.

Alicious mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), aliyezaliwa Jimbo la Kivu, alihamia na familia yake nchini Kenya wakati akiwa na miaka minne na kwa sasa yuko nchini Sweden kimasomo.

Mbali na Posa ya Bolingo, nyimbo nyingine za Alicious ni ‘Niko Poa’, ‘Mpita Njia’  aliomshirikisha Juliana Kanyamozi wa Uganda, ambazo ameziimba kwa Kiswahili.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam  mwanamuziki wa kujitegemea ‘Solo Artist’ Christian Bella ‘Kijana wa Masauti’ alisema taratibu za kumleta msanii huyo zimekamilika, kinachosubiriwa ni muda tu ufike, ambako viingilio na ukumbi vitatangazwa.

Alisema Alicious ataingia nchini wiki moja kabla na watafanya naye mazoezi ya pamoja ili siku ya Usiku wa Masauti, mashabiki wapate burudani ya hali yajuu.

Bella, alisema Alicious amefurahi kualikwa kuja kunogesha usiku huo, ambako pia ataimba ‘live’ kwenye onyesho hilo ambalo Bella amepanga kuzindua rasmi video ya wimbo wake wa ‘Nashindwa’ aliourekodi nchini Afrika Kusini.

Bella, alisema ana imani kubwa video hiyo ya ‘Nashindwa’ italeta mapinduzi katika muziki wa dansi nchini.

“Katika video hii nimeamua kwenda kurekodi nchini Afrika Kusini nikiwa na imani kwamba, hata muziki wa dansi tunaweza kuleta mageuzi kwa kuingia gharama...Kwanini wasanii wa muziki wa kizazi kipya waweze kutoka nje na sisi tusiweze, hapa mimi nimewadhihirishia kwamba tunaweza,” alisema Bella na kuongeza kuwa video hiyo imegharimu zaidi ya sh. milioni 17.

Aidha, alibainisha kuwa jambo kubwa lililomfanya aende kurekodi video hiyo nchini humo ni kutafuta soko la nje, kwa sababu watayarishaji wa muziki wa nje hasa Afrika Kusini, wana uhusiano mzuri na watangazaji na watayarishaji wa vipindi vya televisheni  kubwa kama Channel O, MTV na nyinginezo, hivyo inakuwa rahisi kwao kuipenyeza albamu ya mwanamuziki waliyemrekodi. 

No comments:

 
 
Blogger Templates