Social Icons

Tuesday, August 13, 2013

PUSH MOBILE KUMWAGA MAGARI AINA YA VITZ TAMASHA LA FIESTA 2013

KAMPUNI ya Push Mobile Media Limited, inatarajiwa kutoa zawadi za magari aina ya Vitz manne na pikipiki 12 kwa mashabiki mbalimbali watakaoshinda bahati nasibu maalumu ya tamasha la Serengeti Fiesta, linalotarajiwa kuzinduliwa Jumamosi mjini Kigoma.

Meneja Masoko na Mauzo wa Push Mobile Media, Rugambo Rodney, alisema kuwa mbali ya magari na pikipiki, pia watatoa zawadi za fedha taslimu sh 100,000 kwa mashabiki hao ambao wanatakiwa kutuma neno Fiesta kwenda namba 15678 ili kushinda gari, pikipiki na fedha taslimu, au wanaweza kushinda tiketi ya VIP kwa kutuma jina la msanii kwa mfano Diamond na kuacha nafasi na baadaye kuweka maoni kwenda namba hiyohiyo.

Rodney alisema mbali ya kushinda tiketi, mshiriki atalipiwa tiketi ya ndege kuja Dar es Salaam kwa ajili ya kushiriki tamasha la Fiesta la mwisho.

Alisema kuwa wameamua kuweka zawadi hizo nono ili kunogesha zaidi tamasha hilo, ili kuwanufaisha mashabiki wa muziki hapa nchini.

Aliongeza kuwa wamejipanga ili kuwashirikisha wananchi katika tamasha hilo, kwani pia watazindua huduma mpya ijulikanayo kwa jina la ‘Simu TV’ ambapo itamwezesha shabiki kuona video za muziki na matukio mengine, kupata nyimbo, taarifa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na za michezo kupitia simu ya mkononi.

Kuhusiana na zawadi za fedha, Rodney alisema kuwa itakuwa ikitolewa kila siku kwa mashabiki watakaoshinda bahati nasibu hiyo ambapo jumla ya sh milioni 80 zimetengwa kwa ajili ya programu hiyo itakayodumu kwa miezi mitatu.

No comments:

 
 
Blogger Templates