Social Icons

Tuesday, December 28, 2010

BAADA YA MGANGA KUFARIKI POWER KAPALATA AGEUKIA UDEREVA

POWER Kapalata akiwa kazini kama alivykutwa na Mwandishi wetu Picha/Habari na John Bukuku kwa habari zaidi mtembelee www.Fullshangwe.blogspot.com.
Na John Bukuku/Fullshangwe
Nimeukubali usemao kazi ni popote! Ninaukubali usemi huu kutokana na niliyoyafanya kwenye basi la Sumry High Class wakati nikitokea mjini Sumbawanga Mkoani Rukwa nikienda Mkoani Mbeya ambapo nilipanda basi hilo linaloendeshwa na Dereva Andrew Kapalata maarufu kama (Power Kapalata).
Tulipofika kijiji cha Kaengeza tulikuta mteremko na mlima mkali mvua ilikuwa imenyesha sana usiku na pia katika eneo hilo kuna roli lilikuwa limeharibika, Nilimsikia Dereva Kapalata akimwambia msaidizi wake “Ngoja tuipandishe Kikamanda” aliweka gia namba mbili na akaanza kuondoka huku akizungusha usukani
Nilipomuuliza kwa nini unafanya hivyo alinijibu “Unapofanya hivi gari haiwezi kupoteza mwelekeo kwa utelezi kwani Excell za nyuma na za mbele zote kwa pamoja zinakuwa zinakata utelezi hivyo gari inapanda kirahisi tofauti na kutuliza usukani ambapo gari inakuwa rahisi kupoteza mwelekeo kwa utelezi”
Wakati tunaondoka Mjini Sumbawanga dereva huyo alikuwa ameweka kanda yenye Nyimbo za Mwanamuziki Marehemu Hemedi Maneti 'Sauti ya Chiriku' ambaye alikuwa ni mwimbaji wa bendi ya Vijana Jazz katika miaka ya 1980 na kuendelea.
Nyimbo za mwanamuziki huyo zilivuta sana hisia zangu kiasi ambacho ilibidi nianze kumzungumzia mwanamuziki huyo aliyefariki mwanzoni mwa miaka ya 1990 , Katika mazungumzo hayo Dereva huyo aliunga mkono na kusema, Ah nilikuwa namfahamu sana Maneti alikuwa mtu wangu wa karibu sana mpaka nyumba yao iliyoko kijijini Chala Sumbawanga vijijini naijua na alikuwa akija kupiga muziki Sumbawanga sisi ndiyo tunakuwa watu wake wa Usalama.
Jambo hili lilinivutia sana ikabidi niamue kufanya mahojiani maalum na dereva huyo humohumo kwenye basi, Nilianza kumuuliza mambo mengi juu ya maisha yake na nini anafannya kwa sasa Power Kapalata akasimulia maisha yake hivi “Kwa kusema kweli mimi nilikuwa Mchezaji wa kunyanyua vitu vizito ambapo tumefanya michezo hiyo na wanamichezo wengi sana wakiwemo Power Bukuku, Power Mabula, Power Chiwalala na wengine wengi.

Aliongeza kwamba mchezo huu ulikuwa kama wa miujiza hivi walikuwa na uwezo wa kunyanyua vitu vizito, kuzuia magari, Pikipiki, kunyanyua Kreti tano za bia kwa meno na hata gari lenye uzito wa tani moja na nusu kupita juu ya mkono bila kuvunja mfupa, Wanayanyua vitu vizito wote karibu nchi nzima tulikwa na mganga wetu huko Muze Sumbawanga vijijini akiitwa Pascal Kamoja ambaye alikuwa akitupa dawa ya kunywa na kupaka mwilini.

Mganga huyu alikuwa na uwezo wa ajabu kimiujiza na kila tulipokuwa na mchezo tulikuwa tukienda kumuona na anatupa dawa alafu tunaenda kwenye michezo yetu na ilikuwa ukitumia tu dawa yake mwili unaumuka unakuwa na nguvu ya ajabu na watu wanakuogopa manake unakua unatisha kama Simba.
Power Kapalata anasema pia alikuwa bingwa wa kula katika ukanda wa nyanda za juu kusini ambapo alishikilia ubingwa huo kwa muda wa miaka 12 akinywa vikombe 40 vya chai, Vitumbua 30 na sahani 6 za wali.

Anaongeza kuwa kutokana na kucheza michezo hiyo na kula sana wachumba wengi walimkimbia kila akiweka mambo sawa kesho yule mchumba anapewa taarifa zangu akipewa anakuja kuhakikisha akishuhudia jinsi ninavyokula basi kesho hanitaki tena wachumba zaidi ya wanne walinikimbia mpaka nilipompata mchumba watano ambaye alisema mimi namtaka huyu anayekula sana nikamuoa na sasa tuna watoto wanne

Anasema Mganga wao alifariki mwaka 1993 na michezo ya kunyanyua vitu vizito iliishia hapo na ndipo ikaibuka michezo ya kutunisha misuli ambayo inaendelea mpaka sasa, anaongeza kwamba yeye pia alikuwa na kipaji cha ukocha wa mpira wa Netiboli ambapo aliwahi kuwa kocha wa timu ya mkoa wa Rukwa kati ya mwaka 1977 mpaka mwaka 1985 ambapo mwaka 1978 timu yetu ilishiriki mashindano ya taifa mkoani Shinyanga tukaibuka timu bora yenye Nidhamu kwa mikoa zaidi ya 20 iliyoshiriki mashindano hayo.

Andrew Kapalata Power Kapalata amabye kwa sasa ni Dereva wa mabasi ya Sumry High Class anasema ameendesha magari kwa miaka 33 sasa ikiwa ni Maroli makubwa na magari madogo, na mabasi kwa muda wa miaka 9 na ana uzoefu wa kutosha katika kazi yake hiyo.

No comments:

 
 
Blogger Templates