Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Salim Morcase akifafanua jambo mbele ya Waandishi wa Habari hawapo pichani leo tarehe 20 Januari 2025.
Kibaha ,Pwani
Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia mtu mmoja (jina kapuni) kwa kosa la kusambaza picha mjongeo kwenye mitandao ya kijamii kwa lengo la kuichafua Shule ya Sekondari BAOBAB iliyopo Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo tarehe 20 Januari 2025 kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisini kwake ACP Salim Morcase amesema kuwa Januari 3 ,2025 walipokea malalamiko kutoka kwa uongozi wa shule ya Baobab kuhusu kusambazwa picha chafu katika mitandao ya kijamii picha za mjongeo za utupu na zenye maudhui machafu kimaadili na kinyume na sheria za nchi.
"Picha hizo chafu na zisizo na maadadili imebainika kuwa waliotengeneza waliunganisha na baadhi ya majengo ya Shule ya Baobab ili kuaminisha umma kuwa vitendo hivyo vinafanyika shuleni hapo" amesema Kamanda Morcase.
RPC Morcase amesema kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limefanya uchunguzi na limefanikiwa kumkamata mtu mmoja ambaye uchunguzi wa kitaalam umesaidia kumfikia na kumkuta na picha hizo pamoja na kifaa cha kieletroniki ambacho alikuwa akikitumia kusambaza picha hizo chafu.
ACP Morcase amesema kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linaendelea kuwasaka watu wengine waliohusika katika kutengeneza na kusambaza picha hizo mjongeo.
RPC Morcase amesema kuwa Jeshi la Polisi Pwani wanatoa onyo kwa watu wenye tabia kama hizo za kutengeneza na kusambaza picha kama hizo kwa malengo ya kuchafua wengine au taasisi kwani mkono wa sheria lazima utawafikia na hata kama hautawafikia mapema wataendelea kupata shida ya kujificha na kuacha kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo.
Wakati huohuo Mkurugenzi wa Taasisi ya Baobab Shani Khalfan Swai amesema kuwa taarifa hizo zimewaathiri kwa kiasi japo muitikio wa wazazi kupeleka wanafunzi Shuleni hapo ni mkubwa.
Wakati huohuo Mkurugenzi huyo amesema kuwa kusambaa kwa picha hizo chafu za mjongeo ziliwapa taharuki kubwa wao uongozi wa shule pamoja na wazazi kwani simu zilikua za moto jambo lililowafanya waamue kukaa kimya huku wakitafakari njia sahihi ya kujisafisha na kubainisha ukweli ndipo walipotoa taarifa kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani ambao wanauwezo wa kufanya uchunguzi na jambo la kushukuru kwa upande wao waliposikia mtu mmoja mwenye nia ovu anashikiliwa na Jeshi hilo huku uchunguzi ukiendelea.
Swai ameongea hayo leo kwenye mkutano na Waandishi wa Habari waliofika Shuleni hapo.
"Sisi Baobab tunaimani kubwa na Jeshi la Polisi kwamba wataisafisha Taasisi yetu iliyochafuliwa" amesema Shani.
"Wazazi wa wanafunzi walipatwa na taharuki wengi walipiga simu kuhitaji kupewa ufafanuzi na sisi tuliwafafanulia kwamba hakuna tabia chafu hapa shuleni kwetu na hata zile picha mjongeo wale siyo wanafunzi wetu japo kuna picha za mahafali ambazo mdukuzi alizidukua kwenye kurasa zetu za mitandao ya kijamii na akaunganisha.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Baobab Shani Khalfan Swai watano kutoka kushoto akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi wengine wa Taasisi hiyo.
0 Comments