TUME YA JUMUIA YA MADOLA YAZINDUA MAKABURI MAPYA YA ASKARI WA KIHINDI TANGA


Wakazi  wa Usagara Tanga, Joseph Kimani, Martin Kiarie na Ali Hamis  wakiangalia majina  ya askari wa Uingereza na India waliouwawa Tanga wakati wa vita ya kwanza ya Dunia mwaka
1914, jumla ya askari 270 waliuwawa na majina yao kuwekwa na tume ya Jumuiya ya Madola (CWGC)

Mkazi Usagara Tanga, Joseph Kimani, akiangalia majina
  ya askari wa Uingereza na India waliouwawa wakati wa vita ya
  kwanza ya Dunia ambapo jumla ya askari 270 waliuwawa Tanga wakati wa vita hivyo vilivyopiganwa mwaka 1914.Majina hayo yamehifadhiwa na tume ya Jumuiya ya Madola (Commonwealth War Graves Cammission) (CWGC)
TUME ya Jumuiya ya Madola inayosimamia Makaburi ya Vita vya Kwanza vya Dunia (CWGC) inatarajiwa kuzindua hapa makaburi mapya ya askari wa Kihindi waliokufa katika vita hivyo vya kwanza vya dunia.

Akizungumza  na waandishi habari jijini Tanga jana , Ofisa ufundi wa Jumuiya hiyo, Daniel Achini, alisema uzinduzi huo utafanyika mwezi Novemba 11, 2016.

Achini alisema uzinduzi huo utafanywa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo ya CWGC, Victoria Wallace ukishuhudiwa na Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cook na Balozi wa India, Sandeep Arya.

Sherehe hizo pia zitahudhuriwa na Balozi wa Ujerumani, Egon Konchake na viongozi wa Mkoa na Halmashauri ya Jiji la Tanga.

Alisema makaburi hayo mapya yapatayo 62 yamezikwa miili ya askari wa Kihindi waliokufa vitani katika eneo la Jasin kati ya Januari na Julai, 1915.

Makaburi hayo yamejengwa maeneo ya Usagara na Jasin, karibu na jiji.

Kumbukumbu ya makaburi ya Wahindi na yale ya Usagara yaliyoko hapa Tanga ni sehemu tu ya makaburi mengi yanayohudumiwa na Tume hiyo ya CWGC.

Ofisa huyo alieleza kuwa makumbusho ya Jasin, ulikuwa ni mji wa mbele wa kujihami katika pwani ya kaskazini ya mji wa Tanga na ambao ulichukuliwa na Wajerumani mwezi Januari, 1915.
Alisema vikosi vya Jind na Kashmiri ndivyo vilivyoulinda mji, ambao ulitekwa na kuchukuliwa tena na vikosi vya wanajeshi 2,000 wa Kijerumani tarehe 18 Januari, 1915.

Makumbusho ya makaburi ya Tanga ambayo yapo katika eneo la Usagara, yanahifadhi kumbukumbu ya vifo 394 vilivyotokea katika vita vikali vilivyopiganwa katika mji wa Tanga kati 1914 na 1916 baina ya mataifa makubwa ya Uingereza na Ujerumani.

Achini alifafanua kwamba moja ya kazi muhimu ya Tume hiyo barani Afrika ni pamoja na kutunza makaburi na kumbukumbu za vifo zaidi 190,000 vilivyotokea katika vita vya kwanza na pili vya dunia katika nchi zaidi ya 40 zilizopo Afrika.

"Nchini Tanzania, tunavikumbuka vifo zaidi ya 55,000 vilivyotokea katika vita vyote katika viwanja 12 vya makaburi", alidokeza Achini.

Alitaja baadhi ya maeneo ya makaburi yanayohudumiwa na CWGC yanapatikana Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Iringa na Moshi Zanzibar.

Post a Comment

0 Comments