NA LILIAN LUNDO , MAELEZO
Jumla
ya ombaomba sitini (60) wamekamatwa katika msako wa ombaomba unaoendelea katika
jiji la Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa jana na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar
es Salaam Dkt. Grace Magembe alipokuwa akitoa
majibu ya uwepo wa ombaomba katika jiji la Dar es Salaam licha ya kuwepo kwa
operesheni ya kuwaondoa.
“Zoezi la ukamataji wa ombaomba katika jiji la Dar
es Salaam linaendelea na ombaomba sitini wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka,
wakiwemo watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 ambao wamepelekwa katika vituo
vya watoto yatima kikiwemo kituo cha Kurasini,” alifafanua Dkt. Magembe.
Dkt. Magembe alisema kuwa bado ombaomba wamekuwa
wakionekana ndani ya Jiji la Dar es Salaam kutokana na kuwepo kwa watu wanaotoka
mikoani na kuingia katika makundi ya ombaomba kila siku.
Aidha, aliendelea kwa kusema kuwa kutokana na
kuwepo na ongezeko kubwa la watu wanaotoka mikoani na kujiingiza katika makundi
ya ombaomba, uongozi wa mkoa wa Dar es Salaam unashirikiana na Wizara ya Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kutoa elimu mikoani juu ya operesheni
ya kuondoa ombaomba katika jiji la Dar es Salaam wanaosababishwa na watu wanaokuja
kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.
Mapema Aprili mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam Mhe. Paul Makonda alitangaza oparesheni kubwa ya kuondoa ombaomba katika
Jiji la Dar es Salaam, ambapo alilitaka Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na
Ustawi wa Jamii kufanya zoezi la kuwaondoa ombaomba wote waliopo Jijini humo.
Aidha, Mhe. Makonda amepiga marufuku wananchi
wanaotoa fedha kwa ombaomba kuacha mara
moja ili wajitafutie fedha wao wenyewe aidha kwa kufanya biashara au kurudi
mikoani na kujishughulisha na Kilimo.
0 Comments