Social Icons

Wednesday, April 12, 2017

RAIS DKT. MAGUFULI AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA RELI YA KISASASTANDARD GAUGE DAR HADI MOROGORO


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiangalia kibao cha jiwe la msingi cha Ujenzi wa Reli ya Kisasa Standard Gauge itakayoanzia jijini Dar es Salaam hadi mkoani Morogoro na baadaye kuendelea hadi Kigoma na Mwanza.
Uzinduzi huo umeshuhudiwa na  Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mabarawa, Mama Janeth Magufuli na Mkurugenzi  Mtendaji wa RAHCO Masanja  Kadogosa.

Viongozi wengine waluoshuhudia  ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaa Paul Makonda Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Miundombinu Profesa Norman Sigala , Hawa  Ghasia (Mb) na Mufti Mkuu wa Tanzania Shekhe Abubakary Zubeiry .(PICHA NA IKULU).
         

Na  Immaculate Makilika- MAELEZO

Tanzania inatarajiwa kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuwa na reli ya kisasa inayotumia umeme na mafuta itakayokuwa na uwezo wa kusafiri  masafa marefu kwa mwendokasi wa kilometa 160 kwa saa.

Akizungumza leo katika uwekaji wa jiwe la msingi wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo ya leo huko Pugu nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alisema kuwa reli hiyo itakuwa ya kisasa zaidi barani Afrika na itasaidia kukuza uchumi wa nchi kwa kuchochea fursa za biashara ndani na nje ya nchi.

Awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo ambayo itahusisha kipande cha kilomita 300 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro utagharimu jumla ya shilingi trilioni 2.8 na utatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 30.

Dkt Magufuli alitoa mfano wa nchi zenye reli za mwendokasi lakini masafa mafupi barani Afrika kuwa ni Morocco ambayo inasafiri kwa mwendokasi wa kilomita 220 kwa saa na Afrika Kusini inayosafiri mwendokasi 150 kwa saa.

Dkt Magufuli alieleza kuwa baada ya kukamilika kwa mradi huo Tanzania itakuwa nchi ya kwanza kuwa na treni itakayosafiri masafa marefu kwa mwendokasi wa km 160 kwa saa.

Alifananua kuwa mradi huo wa ujenzi wa reli unatekelezwa kwa fedha za Tanzania ambapo tayari serikali imeshawalipa wakandarasi malipo ya awamu ya jumla ya shilingi bilioni 300.

Akizungumzia umuhimu wa ujenzi wa reli hiyo, Rais Magufuli alisema kuwa reli hiyo itasaidia kuongeza kasi ya usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam kwa haraka na kuwafikia wateja ndani ya muda mfupi.

Vilevile, reli hiyo itarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo pamoja na kukuza biashara kati ya Tanzania na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudani ya Kusini.

Sambamba na hayo, Rais Magufuli alisema kuwa ujenzi wa reli hiyo utasaidia kuimarisha sekta nyingine za uchumi ikiwemo utalii, viwanda, kilimo, pamoja na kutoa ajira kwa watanzania ambapo kutakuwa na ajira muda zipatazo 600,000, na ajira za kudumu 30,000.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema kuwa reli hiyo ya kisasa inayojengwa na wakandarasi kutoka muungano  wa kampuni mbili za nchi ya Uturuki na  Ureno  itakuwa na uwezo wa kusafirisha mizigo tani 10,000 kwa mara moja  na kutumia saa 2 kutoka Dar es salaam hadi Dodoma na saa 7 na dakika 40 kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.

Naye, Mjumbe wa Bodi ya Kampuni ya ujenzi kutoka Uturuki ya Yapi Merkezi Bw.  Emre Aykar alisema kuwa reli hiyo itaimarisha zaidi uhusiano wa Uturuki na Tanzania na kuongeza kiwango cha shughuli za biashara nchini.

“Tunaahidi kujitahidi kumaliza mradi kwa wakati na katika kiwango kinachotakiwa” alisema Bwana Aykar.

Reli hiyo ya kisasa inatarajiwa kujengwa pembeni ya reli ya kati ambayo ilijengwa wakati wa utawala wa kikoloni wa Wajerumani na Waingereza miaka 112 iliyopita.

                           

No comments:

 
 
Blogger Templates