Social Icons

Tuesday, November 8, 2016

KAMBI YA UPINZANI WAUKUBALI MUSWADA WA SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI

Na Mwandishi wetu, Dodoma

Kambi Rasmi ya upinzani Bungeni yaikubali Bodi ya Ithibati, Baraza Huru la Habari pamoja na Bima ya Afya kwa waandishi wa habari nchini.

Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni mjini Dodoma, Msemaji Mkuu wa Kambi hiyo katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Joseph Mbilinyi amesema kuwa Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa 2016 unamaufaa kwa wanahabari nchini “Kifungu cha 58 kinatoa jukumu na kuwataka waajiri wa waandishi wa habarikuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanakuwa na bima ya afya pamoja na kuhakikisha kuwa wanachangia katika mifuko ya hifadhi za jamii” alisema Mbilinyi.

Msemaji huyo aliendelea kusema “Jambo hili ni jema sana na Kambi Rasmi ya Upinzani inaliunga mkono”.

Kuanzishwa kwa Bodi ya Ithibati pamoja na Baraza Huru la Habari ni jambo jema vitu ambavyo vitalinda maslahi ya mwandishi wa habari kwa kuzingatia kuwa moja ya kazi Baraza na Bodi ni kuweka viwango vya uangalizi pamoja na utaratibu wa kitaaluma katika kuratibu tasnia ya habari nchini.

Mbilinyi ametoa rai kwa Wabunge wote bila kujali itikadi za vyama kutambua kuwa jukumu la kutunga sheria ni wajibu wao wa kikatiba ambayo wanawajibika wakiwa sehemu ya Bunge kufanya kazi kwa maslahi mapana ya taifa.

Aidha, Mbilinyi amesisitiza kuwa katika Mkutano wa Nne wa Bunge la 11 Septemba 15 mwaka huu, Serikali ilileta Muswada wa Huduma za Habari na kusomwa mara ya kwanza kwa lengo la kuwapa nafasi Wabunge pamoja na wadau mbalimbali wa habari kupitia na kuufanyia tafakuri ya kina na hatimaye kutoa ushauri kwa Serikali kuhusu Muswada huo.
Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye amesema kuwa mageuzi katika tasnia ya habari nchini yataifanya kuwa taaluma kamili itakayowaletea heshima wanahabari na taifa kwa ujumla.

Kupitishwa kwa Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari itatoa wigo mpana kwa wanahabari kutekeleza majukumu yao kw uhuru ya kukusanya, kuhariri na kuchapisha au kutangaza habari.

Waziri Nape ameongeza kuwa pamoja na maboresho mengi ya Muswada huo pia unzingatia suala la mitambo ya kuchapisha magazeti na majarida nalo limepewa uzito unaostahili kwa kutohusika moja kwa moja kwa kosa la gazeti ambalo limechapisha habari yenye makosa ya kisheria dhidi ya watu au taasisi mbalimbali.

Akinukuu maneno mbalimbali ya watu maarufu duniani juu ya masuala  ya habari 
Msemaji wa Kambi ya Upinzani Mh. Joseph Mbilinyi akizungumza Bungeni.

 Rais wa Marekani Thomas Jefferson Januari 16, 1789, Rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela, Muasisi wa Taifa la India Mahatma Ghandhi, Baba wa Uhuru wa Habari John Stuart Mill (1806-1873) pamoja na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Waziri Nape alimesma kuwa mmoja wa viongozi hao Mahatma Ghandhi aliamini kuwa uhuru wa kweli wa kujieleza ni ule unaoweka mbele heshima ya watu wengine na kuwalinda dhidi ya dhara, kebehi, kejeli na madhara mengine huku Baba wa Uhuru wa Habari John Stuart Mill akibainisha dhima ya uhuru wa vyombo vya habari na umuhimu wa kuwa huriu unapaswa kuzingatia ukomo wa haki ya kupata habari kuwa unakoma pale haki za watu wengine zinapoanzia.

Akichangia katika mjadala wa Muswada huo wakati, Mbunge Sixtus Mapunda amesema kuwa kwa muda mrefu tasnia ya habari haikuwahi kupata hadhi inayostahili ndani ya nchi pamoja na kazi nzuri ya kuhabarisha, kufundisha, kukosoa na kuwasaidia watu watu wenye matatizo wenye changamoto mbalimbali hata kufikia hadhi ya kuitwa muhimili wan ne wa dola.

“Tasnia hii haikuwahi kulindwa, tasnia hii haikuwahi kuenziwa, tasnia hii haikuwahi kuheshimiwa inayostahili, kwa mwandishi wa habari mwenyewe, kwa chombo cha habari na wamiliki wa chombo cha habari tofauti na tasnia nyingine nyingine, kwa mara ya kwanza ndani ya nchi hii, heshima ya tasnia inapatikana” alisema Mapunda.
Mapunda ameitaja tasni hizo kuwa ni za Madaktari, Wahasibu na Wahandisi ambao wanachombo chao kinacholinda maslahi yao, maadili yao na kinachowalinda ili kuendelea kulinda taaluma yao.

Aidha, Mapunda amesema kuwa kwa miaka miaka zaidi ya 23, Muswada utasaidia kutatua matatizo yote yaliyokuwa yanatokana na mapungufu ya Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 kwa kuwa na Bodi ya Ithibati, Baraza Huru la Habari, Bodi ya Ithibati Mfuko wa Mafunzo ambayo ni mambo mapya.

Zaidi ya hayo, Mapunda aliongeza kuwa watu wenye vipaji vya kuandika habari kulingana na taaluma zao ikiwemo uchumi hawajazuiliwa na Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016.

Chimbuko la Muswada huo linatokana na baadhi ya vipengele vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kufanyiwa marekebisho mwaka 1984 ambapo haki ya kikatiba ya kutafuta, kupokea na kutoa habari imeainishwa kwenye Ibara ya 18 (b) pamoja na mikataba mbalimbali ya kimataifa ya inayoainisha haki na wajibu wa sekta ya habari. Mkataba huo wa Kimataifa ni ule wa Haki za Kisiasa na Kiraia wa mwaka 1966 ambao Tanzania iliuridhia Juni 11, 1984 pamoja na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu 1981 ambao nao uliridhiwa Februari 18, 1984.

No comments:

 
 
Blogger Templates