Social Icons

Thursday, October 27, 2016

TANZANIA YAIKARIBISHA KOREA KUSINI KUWEKEZA NCHINI

Na Benny Mwaipaja,WFM, Seoul, Korea

Wafanyabiashara wakubwa kutoka  nchi  ya Korea Kusini, wamekaribishwa kuja kuwekeza nchini Tanzania katika sekta ya viwanda vitakavyoongeza thamani ya bidhaa za kilimo, mifugo, mazao ya bahari pamoja na kutumia malighafi zinazopatikana nchini ili kusisimua uchumi wa taifa na kukuza ajira.

Wito huo umetolewa Jijini Seoul nchini Korea, na Mkurugenzi wa Uhamasishaji uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC, John Mnali  wakati akiwasilisha mada kuhusu fursa za uwekezaji zinazopatikana Tanzania, wakati wa mkutano wa 5 wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Korea ya Kusini na nchi za Afrika(KOAFEC).

Mnali amesema kuwa Tanzania imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwemo kuondoa urasimu wa upatikanaji wa vibali vya kuwekeza na ardhi kwa ajili ya uwekezaji huo ili kuvutia mitaji na teknolojia kutoka nje ya mipaka yake.

Amewashauri wawekezaji hao kufufua viwanda ambavyo havifanyi vizuri nchini, ili kuanza uzalishaji wa bidhaa zitakazotumia malighafi zinazopatikana nchini pamoja na kutumia soko kubwa lililopo katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na soko la AGOA la Marekani.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Utafutaji Rasilimali, kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Sabra Issa Machano, amewahimiza wawekezaji wa Korea kwenda kuwekeza Visiwani humo na Tanzania kwa ujumla katika sekta za kilimo, viwanda na uvuvi wa samaki na mwani katika Bahari Kuu ili wakazi wa nchi hiyo na wawekezaji waweze kunufaika na rasilimali zilizoko visiwani humo.

Amewahimiza wawekezaji hao kujenga hoteli za kisasa kwa ajili ya kuhudumia soko la utalii ambalo ni kubwa nchini humo, pamoja na kutumia mandhari ya Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao ni kivutio kikubwa cha watalii baada ya kutangangazwa na Shirika la Kimataifa linaloshughulika na masuala ya sayansi na utamaduni-UNESCO kuwa mji wa urithi wa Dunia.

Baadhi ya wawekezaji ikiwemo kampuni ya Youngsan, inayojihusisha na utengenezaji na usambazaji wa vipuri vya magari pamoja na kampuni ya MarineBio inayojihusisha na biashara ya utengenezaji wa bidhaa zinazotokana na mwani, wameonesha nia ya kuwekeza Tanzania baada ya kuvutiwa na mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania.

“ Kampuni yetu imetafuta kwa muda mrefu fursa ya kuwekeza Tanzania lakini tulikuwa hatufahamu ipasavyo njia za kutumia kufikia uwekezaji huo ambapo sisi tunajihusisha na biashara itokanayo na zao la mwani linalozalishwa kwa wingi Zanzibar ambapo tunatengeneza bidhaa za karatasi, urembo, karatasi na vitu vingine vingi” alisema Yun-Young .

Amesema kuwa wanatarajia kufungua kiwanda kikubwa ambacho kitazalisha ajira kwa wakulima na wafugaji wa samaki nchini Tanzania kwakuwa kampuni yake itajihusisha na biashara kubwa itakayochangia kukuza ajira na kuwafanya watu wengi hususan wanawake, waondokane na umasikini wa kipato.

Katika Mkutano huo uliomalizika leo, Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, ambaye amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ambapo, Tanzania imesaini mkataba mmoja pamoja na Makubaliano ya ushirikiano wa pamoja kwa ya upanuzi wa miundombinu ya maji taka katika Jiji la Dar es salaam na ujenzi wa njia ya umeme yenye msongo wa kV400 kutoka Mbeya, Kigoma hadi Nyakanazi. ​

No comments:

 
 
Blogger Templates