Social Icons

Wednesday, August 31, 2016

TANZANIA YAFANIKIWA KUPUNGUZA IDADI YA WAGONJWA WA TRAKOMA

Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara hiyo Dkt. Magreth Muhando akizungumza kwa niaba ya Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwenye ufunguzi wa Mkutano wa pili wa mwaka wa nchi 7 za Afrika Mashariki zilizo katika mapambano dhidi ya Trakoma unaofanyika jijini Arusha.
Mratibu wa Taifa wa Magonjwa yasiyopewa kipaumbele kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto   Upendo John Mwingira akizungumza wakati wa mkutano wa pili wa mwaka wa nchi 7 za Afrika Mashariki zilizo katika mapambano dhidi ya Trakoma unaofanyika jijini Arusha.
Washiriki wa mkutano huo kutoka nchi 7 za Bara la Afrika wakiwa katika picha ya pamoja.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya kupambana na Trakoma (International Trachoma Initiative) Dkt. Paul Emerson akizungumza katika Mkutano huo  ambapo ameipongeza Tanzania kwa kazi nzuri inayofanya ya kuhakikisha ugonjwa wa Trakoma unatokomezwa.

Na. Aron Msigwa - ARUSHA
.

Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Trakoma (Vikope) kufuatia kupungua kwa idadi ya wagonjwa na maeneo yaliyokuwa yakipata dawa za kutibu ugonjwa huo chini ya Kampeni ya utoaji wa dawa kwa watu wengi (Mass Drug Administration) iliyoanzishwa mwaka 1999.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwenye ufunguzi wa Mkutano wa pili wa mwaka wa nchi 7 za Afrika Mashariki zilizo katika mapambano dhidi ya Trakoma unaofanyika jijini Arusha, Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara hiyo Dkt. Magreth Muhando amesema Tanzania imepata mafanikio hayo kutokana  na juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.

Sasa hivi wilaya 22 tumeziacha kati ya 56 zilizokuwa zikipata dawa chini ya mpango wa kutoa dawa kwa watu wengi ulioanza mwaka 1999, hii kutokana na kupata mafanikio mazuri na tunategemea kupata mafanikio zaidi kwa kuendelea kuzipunguza zilizobaki Amesema.

Ameeleza kuwa kupungua kwa idadi ya wagonjwa Trakoma nchini Tanzania mwaka hadi mwaka kunatokana na juhudi za Serikali na  wadau kupitia afua mbalimbali chini mpango ujulikanao kama SAFE unaohusisha huduma za Upasuaji, utoaji wa dawa za Antibayotiki mapema, kampeni ya kuhamasisha wananchi kuosha uso pamoja na uzingatiaji wa usafi wa mazingira.
 
Dkt. Muhando amebainisha kuwa Trakoma umekuwa chanzo cha upofu na umasikini pale mgonjwa anapochelewa kutibiwa mapema na kusisitiza kuwa lengo la nchi hizo kukutana nchini Tanzania ni kuweka mkakati wa pamoja wa ushirikiano juu ya namna bora ya kudhibiti maabukizi ya ugonjwa huo kutoka sehemu moja hadi nyingine kutokana sababu za kijiografia na mwingiliano wa watu kutoka nchi moja moja hadi nyingine hali inayoweza kuchangia kusambaza ugonjwa huo.

Amesisitiza kuwa bado watanzania wanalojukumu la kuhakikisha ugonjwa huo unatoweka katika maeneo yao kwa kuzingatia na kufuata kanuni za afya, kufanya usafi wa mwili hususan uso kila siku kwa maji safi na sabuni pamoja na kufanya usafi wa mazingira ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.

Tumeona ni muhimu nchi hizi saba  za Tanzania, Kenya, Eritera, Sudani, Sudani ya Kusini, Uganda na Ethiopia kushirikiana kikamilifu katika mpango wa kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa vikope kwa sababu watu wa nchi hizi hutembeleana kutoka sehemu moja hadi nyingine, tusipokuwa na njia mahususi za pamoja za udhibiti ugonjwa huu unaweza kuendelea kusambaa” Amesisitiza.

Ameongeza kuwa kazi inayofanywa sasa na nchi hizo ni kuendelea kutoa elimu hasa kwenye maeneo ambayo yana madhara ya ugonjwa huo kuielimisha jamii kutambua kuwa tatizo hilo lipo na jamii zinazoishi kwenye halmashauri zenye matatizo hayo kuendelea kupewa elimu dhidi ya kinga pia kuwahimiza wananchi kuzingatia usafi kama njia pekee ya kujikinga na ugonjwa huo, kuhakikisha tiba ya ugonjwa huo inapatikana pamoja na kuwaelimisha wale waliopata madhara ya ugonjwa huo ambao wanatakiwa kufanyiwa upasuaji kuwa tayari kwa tiba hiyo.

Dkt. Muhando amewashukuru wadau mbalimbali wa maendeleo kwa kuendelea kutambua mchango wa Tanzania katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyopewa kipaumbele pamoja na kutimiza malengo ya kidunia ambayo yanatoa wito kwa Tanzania kuwa imeondoa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2020.

 Aidha, amezitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili kampeni ya kuwafikia wale walioathirika katika maeneo yenye maambukizi ya ugonjwa huo kuwa ni pamoja na maeneo ya jamii za wafugaji kuwa katoka mwingiliano mkubwa kutokana na sababu za mazingira hali inayohitaji nguvu kubwa za udhibiti baina ya nchi husika.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya kupambana na Trakoma (International Trachoma Initiative) Dkt. Paul Emerson akizungumza katika Mkutano huo ameipongeza Tanzania kwa kazi nzuri inayofanya ya kuhakikisha ugonjwa wa Trakoma unatokomezwa.
Amesema kuwa yeye kama Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya Kupambana na Trakoma (ITI) amefurahishwa na na kuridhishwa na  kazi nzuri inayofanywa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto ya Tanzania pamoja na juhudi za kuendelea kuwaelimisha wananchi na kutoa tiba katika maeneo  yanakabiliwa na ugonjwa huo.

Aidha, amesema katika bara la Afrika maeneo ambayo yana vita na mapigano bado yanakabiliwa na kiwango kikubwa cha maabukizi ya  ugonjwa huo huku akizitaja nchi za Ethiopia, Sudani ya Kusini, Sudan, Uganda na Kenya kuwa miongozni mwa nchi za bara hilo zenye idadi kubwa ya wagonjwa wa Trakoma.

Kwa upande wake Mratibu wa Taifa wa Magonjwa yasiyopewa kipaumbele kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto   Upendo John Mwingira akizungumza wakati wa mkutano huo amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache za Bara la Afrika ambazo zimepata mafanikio katika utokomezaji wa ugonjwa wa Trakoma tangu kuanza kwa mpango maalumu wa kupambana na ugonjwa huo mwaka 1999. 

Amesema ugonjwa wa Trakoma/Vikope nchini Tanzania kwa mujibu wa Takwimu uko katika wilaya 56 na kueleza kuwa juhudi ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Serikali kukabiliana nao hali iliyochangia maabukizi mapya kudhibitiwa katika wilaya 22 ambako wananchi hawahitaji tena  dawa.

Amewatoa hofu wananchi kuhusu matibabu ya Trakoma kwa kuwaomba wale ambao kope zao zimeathirika kujitokeza ili waweze kufanyiwa huduma ya upasuaji ambayo inamuwezesha mgonjwa kurudi katika hali yake ya kawaida.

Natoa wito kwa wagonjwa wajitokeze wasiogope, ni jambo linalofanyika kwa utaalamu wa hali ya juu na mtu akifanyiwa urekebishaji wa kope anarudi na kuweza kuona kama kawaida
Aidha amesema kuwa licha ya  halmashauri nyingi za Tanzania kipata mafanikio katika kudhibiti hali ya maambukizi ya ugonjwa huo bado maeneo ya jamii za wafugaji hasa wilaya za Longido, Monduli na Ngorongoro bado zina maambukizi hali inayohitaji ushirikiano wa udhibiti wa tatizo hilo kati ya Tanzania na Kenya.

 Kwenye mafanikio huwezi kukosa changamoto, Tanzania maambukizi yamepungua halmashauri nyingi kiwango cha maambukizi kimepungua isipokuwa kwenye jamii zile za wafugaji wa jamii ya maasai kwenye wilaya tatu za Longido, Monduli na Ngorongoro ambapo tunahitaji juhudi za pamoja kati yetu na Kenya kwa kuwa kuna mwingiliano mkubwa baina ya watu wa maeneo haya na ndiyo maana tumekutana Amesisitiza. 

Kuhusu hali ya maambukizi ameyataja maeneo yenye ukame na yale yenye shida ya maji yaliyo mkoa wa Manyara na Dodoma kuwa bado yanakabiliwa na tatizo hilo na kuongeza baadhiya maeneo ya Arusha , Manyara, Dodoma katika wilaya ya Kongwa, Chemba na Chamwino yanahitaji huduma ya dawa.

Kuhusu takwimu za hali ya maambukizi nchini amesema kuwa takribani watu 160,000 wameambukizwa huo na kubainisha kwamba kupitia mikakati mbalimbali ya Wizara na wadau mbalimbali wameweza kuendesha  huduma ya upasuaji kwa wagonjwa wenye tatizo hilo 80,000.

No comments:

 
 
Blogger Templates