Social Icons

Monday, August 29, 2016

SERIKALI YAFUNGIA VITUO VYA REDIO VYA MAGIC FM NA REDIO 5 YA ARUSHA



Serikali   imevifungia vituo viwili vya redio nchini kutokana na kurusha hewani taarifa za kichochezi zinazoweza kuchangia uvunjifu wa amani.

Tamko la kufungwa kwa vituo hivyo vya  redio limetolewa  jana Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Utamaduni ,Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye alipokuwa akizungumza  na waandishi wa habari.

Nape alivitaja vituo hivyo kuwa ni Kituo cha Redio Five cha Arusha na Kituo cha Redio Magic  FM Dar es Salaam na alisisitiza kuwa utekelezaji wa tamko hilo umeanza  jana Agosti 29, 2016 mara baada ya kutangazwa.

“Uamuzi wa kuvifungia vituo hivyo umefikia baada ya kujiridhisha kuwa kipindi cha MATUKIO kilichorushwa tarehe 25 Agosti ,2016 muda wa 02:00 usiku hadi 03:00 usiku  na Kituo cha Utangazaji cha  Redio Five  Arusha na kipindi cha cha Morning  Magic katika kipengele cha KUPAKA RANGI kilichorushwa tarehe 17 Agosti, 2016 kati ya saa 01:00 asubuhi na saa 02:00 asubuhi vilikuwa na maudhui ya uchochezi unaoweza kuleta uvunjifu wa amani na hivyo kukiuka masharti ya kanuni ya 5 (a),(b),(c) na (d) pamoja na Kanuni ya Huduma za Utangazaji (Maudhui) za mwaka 2005”, alisema  Nnauye.


Waziri huyo mwenye dhamana na vyombo vya habari nchini alisema vituo hivyo vimefungiwa kwa muda usiojulikana na ameelekeza  Kamati ya Maudhui kuviita vyombo hivyo na  kuwasikiliza kwa kina zaidi na kumshauri hatua zaidi za kuchukua kwa mujibu wa Kanuni za Utangazaji za mwaka 2005. 

Pamoja na hayo Nape alivitahadharisha  vyombo mbalimbali  vya habari ,kutoshawishika kuvunja Sheria na Kanuni  zinazoongoza tasnia ya Habari ili kulinda heshima ya tasnia ya habari  na kuhakikisha nchi inabaki na amani.

Hata hivyo  Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ya mwaka 2003  Kifungu cha 28 (1) kimempa Mamlaka Waziri wa mwenye dhamana na masuala ya Habari kufungia vyombo vya habari vinavyoweza kurusha hewani habari za uchochezi.

No comments:

 
 
Blogger Templates