Social Icons

Thursday, July 21, 2016

KALA JEREMIAH, SUPER NYAMWELA KUPAMBA MSIMU MPYA WA JUKWAA LA SANAA LA BASATA



Ofisa Habari wa BASATA , Aristides Kwizera

Wasanii Kala Jeremiah na Super Nyamwela wanatarajiwa kupamba msimu mpya wa programu ya Jukwaa la Sanaa ambayo imekuwa ikiendeshwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na chama cha waandishi wa habari za Sanaa na Utamaduni (CAJAtz) kwa miaka mitano sasa tangu mwaka 2011.

Msimu mpya wa Jukwaa la Sanaa unatazamiwa kuzinduliwa rasmi Jumatatu ya tarehe 25/07/2015 kwenye Ukumbi wa BASATA ulioko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam kuanzia saa saa 4:00 Asubuhi – 6:30 Mchana.

Wasanii hawa wanatarajiwa kuupamba uzinduzi huo kwa kutoa burudani mbalimbali sambamba na kuongea na wasanii wachanga katika kuwahamasisha na kuwajengea uwezo juu ya namna wanaweza kutumia fursa mbalimbali za mashindano ya kukuza vipaji katika kujijenga kisanaa.

BASATA linatambua kwamba kumekuwa na tatizo la wasanii katika kutambua na kuchangamkia fursa mbalimbali zilizoko katika sekta ya Sanaa hasa zile zilizomo kwenye mashindano mbalimbali ya kutafuta vipaji ambayo wasanii Kala Jeremiah na Super Nyamwela wamekuwa wakishiriki kikamilifu.

Ushiriki wa wasanii hawa katika kuwajengea hamasa na kuwapa changamoto wasanii wachanga utasadia katika kuwajengea uwezo wa kutumia fursa hizo.

Mbali na burudani na elimu hiyo, uzinduzi huu wa msimu wa mpya wa Jukwaa la Sanaa unaotarajiwa kuhudhuriwa na watu zaidi ya mia moja (100) utahusisha pia kongamano maalum ambalo litajikita katika kutoa elimu mbalimbali kuhusu sekta ya Sanaa kwa wadau watakaohudhuria. 

Jukwaa la Sanaa ni programu iliyobuniwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa lengo la kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo sekta ya Sanaa lakini pia kusaidia waandishi wa habari kupata habari zihusuzo sekta ya Sanaa kutoka vyanzo mahsusi.

Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini

Imetolewa na Kitengo cha Habari
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)

No comments:

 
 
Blogger Templates