Social Icons

Tuesday, July 12, 2016

JERRY MURO , HAJJI MANARA KIVUTIO MSIBANIHajji ambaye ni mtoto wa kiungo mahiri wa Yanga, Pan African na Taifa Stars, alianza  maneno yake yaliyoanza kuamsha walio msibani kumsogelea kwa kusema atamuagiza mdogo wake Jerry aende  Morogoro kumwakilisha kwenye mazishi  na klabu ya Simba itatoa ubani wa kiasi cha sh. 500,000, ambazo Murro atakwenda kuzikabidhi kwa familia. 

“Niko hapa kwa niaba ya Rais wa Klabu ya Simba Evans Aveva  , hivyo kwa niaba yake na wanachama wa Simba  tumekumbwa na  msiba mzito  hivyo  hakuna jambo jingine la kusema bali ni kumuombea kwa Mwenyezi Mungu aipokee roho ya marehemu  na ampumzishe kwa amani” alisema Manara.

Aidha aliwavunja mbavu zaidi  mamia ya watu waliokuwa msibani baada ya kusema kwamba anamjua mdogowake Jerry Murro kwa kupenda kwake sifa na ushindani akija atatangaza kiasi kikubwa zaidi ya kile kilichotolewa na Simba.

Murro ambaye alikuwepo msibani mapema kabisa, alianza kwa kusema “kwa niaba ya  ya Rais , wanachama , wapenzi wa  Klabu ya Yanga,ningependa kuwafahamisha kwamba mume wa Eliza  ni shabiki na mwanachama wa  klabu yetu ya Yanga, hivyo mbali ya kumpoteza mwanahabari mwenzetu lakini pia tumempoteza shemeji” 

Murro aliendelea kwa kusema kuwa Eliza alikuwa  kiungo muhimu  na sisi wana Yanga tunatambua  na kuuthamini mchango alioutoa  kwa klabu yetu  ila kulikuwa na siri moja ambayo ilimpa wakati mgumu sana  marehemu katika enzi za uhai wake ndani ya miaka minne iliyopita, kwani alilazimika kuandika habari za  klabu ya Yanga ambao walikuwa wakiongoza katika ligi ya mabingwa  licha ya yeye kuwa shabiki  na mwanachama mnazi wa Simba.

“Elizabeth alilazimika kuandika habari zetu jinsi tulivyokuwa tuking’ara huku  huku wenzetu wa matopeni  wakiwa wamekwama, sisi  Yanga tutatoa  ubani wa sh. 500,000 pia  tutafanya kama alivyoniagiza  Manara nitaungana wafiwa kwenda kuiwakilisha Simba kwenye mazishi   ya marehemu Mkoani Morogoro ” alisema Muro na kuamsha kicheko kwa wawili hao walipokuwa wamezungumzwa na waombolezaji ambao idadi yao kubwa ni wanahabari wa vyombo  mbalimbali.

Murro alisisitiza kwamba yeye bado ni Msemaji halali wa Yanga  kwa sababu bado hajapata barua rasmi ya kusimamishwa kwake  kutoka Shirikisho la Soka nchini (TFF), na kwamba anaripoti kwa mwajiri wake Yanga kama ilivyo  ajira yake inavyomtaka.

Wakizungumza katika nyakati tofauti ,Manara alikiri kwa kusema kuwa Klabu ya Simba imempoteza  mwandishi habari mahiri ambaye pia alikuwa  mwanachama mwenye kadi ya klabu hiyo. Manara alijiongeza zaidi na kusema pamoja na kwamba wanataniana na Yanga, lakini amezisikia habari za Murro kumtafutia pesa za matibabu kwa mashabiki wa Yanga na kusema ni uungwana unaopaswa kuendeleza na si vinginevyo.

“Ameniambia mdogo wangu Murro wameshafikisha milioni na bado wanachanga, kiukweli huyu dogo ni muungwana, nasubiri atomize ahadi yake, nitazipokea, sisi ni watani na si wagomvi” alisema Manara.

Mbali ya wasemaji hao, nae Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari za  Michezo  Tanzania (TASWA), Juma Pinto alitoa salamu za  rambirambi chama hicho na kusema kuwa “Tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa mwenzetu ambaye ni mwanachama wetu”.

“Mchango wake bado ulikuwa unahitajika , alikuwa mcheshi alijitoa katika kazi zake za kila siku kwa hali na mali  binafsi nilimfahamu  vema namna alivyokuwa akijituma  ipasavyo TASWA inatoa pole  kwa familia na wanatasnia kwa ujumla  kwa kuondokewa na mpendwa wao  kifo hakizuiliki lakini tuna wajibu wa  kumuombea mwenzetu na sisi tunatoa rambirambi kiasi cha sh.500,000” alimalizia Pinto.

Msemaji wa timu ya Ruvu Shooting Masau Bwire alisema kuwa ametumwa kumwalisha Kanali  Charles Mbuge kutoa salamu za rambirambi kiasi cha 300,000 kwa niaba ya timu  yao. Miongoni mwa wa soka waliofika kwenye msiba huo ni pamoja na Mwenyekiti wa Chama Cha Soka Mkoa Dar Es Salaam, Almas Kasongo  Mwenyekiti wa Kamati ya soka la vijana,  Ayoub Nyenzi na Wachezaji wa zamani Ken Mkapa,   Mohemed Hussein Mmachinga na Ramadhan Kampira.

Marehemu Mayemba alizaliwa  Desemba 1980 alikuwa  Kaimu Mhariri Msaidizi wa wa Michezo na Burudani  Katika Kampuni ya Business Times Limited wachapishaji wa  gazeti la Majira .

Mayemba alifariki Jumamosi  iliyopita  saa mbili usiku baada ya kuanguka  ghafla nyumbani kwake Tabata  Kisukuru na alifariki  dunia wakati akiwahishwa  Hospitali ya  Rufaa  ya Amana Jijini Dar es Salaam.

Marehemu ameacha mume na watoto watatu  pia atazikwa leo kwenye makaburi ya Kola Mkoani Morogoro. Bwana Ametoa, Bwana Ametwaa, Jina lake Lihimidiwe.


No comments:

 
 
Blogger Templates