Social Icons

Tuesday, July 12, 2016

KIPINGU: NABII HAKUBALIKI NYUMBANI KWAO

 Kipingu akiwa kwenye picha pamoja na mmoja wa wachezaji wa mcheo huo.
Kipingu akiwa na wanafunzi wake wakiwa wameshinda medali.



NA KHADIJA KALILI, NAIROBI
Kuna usemi usemao nabii hakubaliki nyumbani, ndivyo usemi  huo unavyojidhihirisha kwa Mtanzania Kiango Kipingu, akiwa kocha mahiri wa kutumainiwa kwa Taifa la Kenya. 

Tanzania pamoja na kutokuwa na idadi kubwa ya makocha waliobobea  katika mchezo wa Tenis, bado ameshindwa kukubalika nyumbani na ujzui  wake, kwa sasa unawanufaisha Wakenya.

Bongoweekend Blog ilifanya mahojiano maalum na Kocha huyo kwenye viwanja vya Lunar Park Jijini Nairobi mwishoni mwa wiki na kujinasibu kuwa anafanya kazi zake za kufundisha kucheza mchezo huo jijini hapa kwa nafasi kubwa kiasi kuonyesha  kipaji chake.

 Anajipambanua kwa kusema kuwa yeye ni  Mwalimu wa kutumainiwa katika shule ya  Tennis inayofahamika kwa jina la ACE Tennis Academy analipwa mshahara mnono  kutokana na kazi hiyo.

¨Katika shule hii ambayo licha ya wanafunzi wake kusoma masomo mengina ya kawaida lakini ni maalumu kwa kusaka wanafunzi ambao wana vipaji huku lengo kubwa likiwa ni kupata wawakilishi wa nchi  katika michuano ya mchezo huu” anasema Kipingu.

Akifananisha namna  nchi ya Tanzania na Kenya wanavyo uthamini mchezo huo anasema “hapa  wameweka mfumo  rasmi  wa kuandaa vijana wadogo wenye kipaji cha kucheza mpira wa meza pia huandaa wachezaji wa timu ya Taifa katika ngazi za awali na hii shule ninayofundisha ndiyo kinara katika kutoa  wachezaji wadogo lakini  wenye vipaji katika uchezaji¨ anasema.

Changamoto  alizopitia 
Kipingu anaweka wazi na kusema kuwa  jambo kubwa lililomkimbiza nyumbani  (Tanzania) ni ukata wa fedha na kutothaminika kwa kazi  yake licha ya kuwa na  mchango  mkubwa  alioutoa katika timu za nyumbani ikiwa ni pamoja na kuvumbua na kukuza vipaji vya mchezo huo.

Anasema aliingia Jijini hapa Januari 2015  hapo alipokelewa vizuri na kufanikiwa kusaini  makataba wa miaka  mitatu wa kufanya  kazi hiyo.

¨ Sababu kubwa iliyonileta hapa Nairobi ni kutokana na jinsi wenzetu wanavyo wajali makocha tofauti na ilivyo nyumbani, kwetu hawathamini michezo  na hawajali kuwa michezo ni ajira ambayo inaweza kumtajirisha mtu lakini huku wanaheshimu utaalamu wa aina yeyote ambao mtu anao na kuuendeleza  kama jinsi nilivyojionea kwangu mimi nimethaminiwa ugenini na kudharauliwa nyumbani ¨anasema Kipingu.

Anaongeza kwa kusema kuwa  tofauti iliyopo kati ya nchi mbili hizi ni kuwa  Kenya wamejiwekea utaratibu wa kumthamini mtu na utaalamu wake pamoja kumpa moyo muhusika.

Anaongeza kwa kusema kuwa nchini Kenya wanaipa kipaumbele kikubwa  michezo na ndiyo sababu wamekuwa wakiweza kupata medali nyingi kwenye michuano ya kimataia huku akitolea mfano wa mchezo wa riadha ambao wamekuwa waking’ara kwenye  mashindano mbalimbali.

Anakwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa alipokuwa nyumbani Tanzania alikuwa ni Mtaalamu  wa Ufundi wa mpira wa meza katika Chama Cha Tanzania Tennis Association (TTA), pia alikuwa Msimamizi  wa kueneza mchezo  huo  nchi nzima  huku akiwa amevalia kofia nyingine ya Kocha Mkuu wa Tennis Tanzania.

Anasema licha ya kujitolea kwa hali na mali lakini alikuwa halipwi ujira wowote  licha ya kuwa TTA, walikuwa na mdhamini ambaye alikuwa akitoa fedha  lakini wajanja wachache na wasiopenda  maendeleo ya mchezo huo walikula fedha hizo  na hadi leo bado hajalipwa  chochote.




Kipingu anaweka wazi kwa kusema kuwa wakati akifundisha timu nyumbani Tanzania , aliweza kufanikisha  timu ya Taifa  ya Vijana chini ya umri wa miaka 16 kufanikiwa  kuingia  katika  fainali  za Afrika Mashariki na Kati na kuibuka katika  nafasi ya pili kwenye michuano  hiyo.

“Mimi niliongoza timu  hiyo hadi  ikafanikiwa kushika nafasi ya pili lakini sikulipwa chochote , na hakuna kiongozi yeyote aliyeonesha kujali jitihada zangu katika kuifikisha timu  kwenye nafasi hiyo” anasema Kipingu.

Aidha anaongeza kwa kusema kuwa akiwa nchini Kenya ameweza kupata mafanikio ya kuipeleka  timu ya vijana chini ya umri wa miaka 14 kushiriki kwenye mashindano ya dunia ya mchezo huo yatakayofanyika mjini  Pendevo nchini Serbia.

¨Wakiwa katika michuano hiyo nchini Serbia timu ya tenis Kenya itakutana na timu nyingine  zinazo shiriki  michuano hiyo kutoka nchi mbalimbali  duniani” anasema Kipingu.

Anasema michuano hiyo  ya vijana wadogo hufanyika  kwa kuzingatia kalenda ya shule, michuano hiyo hufanyika wakati wanafunzi wamefunga shule¨ anasema Kipingu.

Matarajio yake  katika siku za usoni
Anasema  kuwepo kwake nchini Kenya  anajifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na  kuiba ujuzi ambao amejipanga kuurudisha nyumbani Tanzania kwa lengo la kuukuza mchezo huo.

Najifunza sana kutoka kutoka kwa  Wakenya, najifunza mawazo yao lakini bado pia nina ndoto ya kurudi nyumbani ili kuukuza mchezo huu.
Anasema kuwa  ana ndoto ya kuja  kuendeleza  mchezo wa Tennis  kutengeneza wachezaji  ambao wataweza kupata ajira kwa kupitia mchezo huo kwani michezo ni ajira.

Anasema  hivi sasa tayari ameshasajili Kampuni yake ambayo  pindi atakapokuwa tayari kurudi nyumbani atakuwa na  mradi wa kusaka vipaji na kuviendeleza,nitakaporudi nyumbani nitakua natafuta vipaji na kuaendeleza.

Nitakaporudi nyumbani nitanzisha shule  maalum ya Tenis  ambayo itatoa elimu  na kuwafundisha vijana .

“Uzuri wa mchezo wa Tenis unaweza ukawa na vijana 50 ambao kati yao ukafanikiwa kuibua  mchezaji mmoja ambaye akaja kuwa nyota mmoja wa wataifa kama vile Serena Williams alivyo tajiri kutokana na kupata mshahara mnono na kuingia mikataba mingi ya matangazo ya biashara  nina imani katika hili  Tanzania inaweza kufanikiwa kuja kupata mchezaji atakayeng’ara kimataifa” anasema Kipingu.

Nasaha zake  kwa serikali
Anazungumza huku akionesha msisitizo  katika hili anaiomba serikali  iliyopo madarakani hivi sasa  itupie jicho la tatu kwenye sekta ya michezo huku akiomba  viongozi wa  juu waweze kubadilishwa endapo  tunataka  kufanya mapinduzi kwenye michezo.

“Mfumo tulioukuta na viongozi  wa michezo kama vile Mkurugenzi wa Michezo Leonard Thadeo angebadilishwa  na nafasi hiyo apewe kijana ili aje na mawazo mapya  itasaidia kuweza kubadili mfumo mzima wa michezo ambao hauna  malengo yoyote ndiyo sababu kubwa Tanzania hatufiki mbali kwenye michezo” anasema Kipingu.

Anaweka wazi kwa nini Thadeo abadilishwe ni kutokana na kushindwa kuipeleka mbali michezo kutokana ubunifu wake wa mikakati ya michezo kufikia ukomo.

“Mimi tangu nilipokuwa kijana mdogo namsikia tu lakini sijaona matunda yeyote aliyoleta  katika michezo nchini” anasema Kipingu.

Anakwenda  mbali zaid kwa kusema  katika michezo kuna fedha  na ajira za kutosha  lakini jambo moja kubwa tunalohitaji ni kujiwekea mikakati madhubuti  ili tuweze kuwafikia walipo wenzetu na nchi nyingine ulimwenguni.

Anasema  yuko tayari   kufanya kazi na kocha yeyote nchini ambaye atajitokeza ikiwa ni katika kuukuza mchezo huu.

Alikotoka
Anasema alipokuwa mwanafunzi  alikuwa anapenda mchezo wa soka na alikuwa akicheza kwa umahiri  kipaji ambacho kilivumbuliwa na kukuzwa na aliyekuwa  Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kijeshi ya Makongo Kanali Mstaafu Idd Kipingu ambaye ni baba yake mdogo.

Lakini alikuja kubadilika baada ya kumshuhudia kaka yake  anayemtaja kwa jina la  Sebastian Mtupili aliyekuwa  bingwa wa Tenis  nchini katika miaka ya nyuma.

Jinsi alivyovutiwa na mchezo huo anasema ilitokana na kwenda kuangalia mechi alizokuwa akilicheza kaka  yake ndipo alipoanza kuupenda mchezo huo.

No comments:

 
 
Blogger Templates