SIKU chache
baada ya msanii wa vichekesho, Steve Mengele ‘Steve Nyerere’ kupigwa ‘stop’
kuendelea na mkutano wake wa hadhara Kinondoni, jijini Dar es Salaam,
kilichomponza kimeanikwa.
Msanii huyo Juni
28 aliitisha mkutano wa hadhara Kata ya Bwawani kuhamasisha vijana
kujiandikisha katika daftari la wapiga kura, lakini akiwa jukwaani Mwenyekiti
wa CCM Tawi la Bwawani, alishika kipaza sauti na kutangaza kuwa amepokea amri
kutoka ngazi za juu kuvunja mkutano huo, huku Steve Nyerere akibaki amepigwa
butwaa.
Habari
kutoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kinondoni, zinaeleza kuwa msanii
huyo alikiuka taratibu kwa kuutumia mkutano huo kutangaza nia kugombea ubunge huku
wakati ukiwa bado haujafika na jimbo hilo likiwa na Mbunge wa CCM, Idd Azzan.
Chanzo hicho
ambacho hakikupenda kutajwa jina kwa kuwa si msemaji rasmi wa chama, kilisema
Steve Nyerere kama Kamanda wa Vijana wa Kata ya Bwawani, alikuwa sahihi
kuhamasisha vijana kujiandikisha kwenye
daftari la mpiga kura, lakini kosa kubwa alilolifanya ni kutangaza nia.
“Kosa
lililomponza na ambalo anaweza hata kushitakiwa kichama, ni kuutumia mkutano
huo kutangaza nia, tena kwa kuongozana na msafara wa magari huku yakiwa na
picha za kuhamasisha zikiwa na ujumbe: ‘Twende na Steve’, huku mwenye jimbo
yupo... Endapo atamshitaki, atakuwa katika wakati mgumu kisiasa,” alisema
kiongozi huyo.
Baadhi ya
wanasiasa wakongwe walieleza kwamba
kitendo chake cha kuitisha mkutano wa hadhara na kuweka mabango ya picha zake
si sahihi, kwa sababu wakati wa kutangaza nia na kuanza kampeni bado.
Mengele
ambaye pia ni msanii wa filamu, alijizolea umaarufu kwa vichekesho na kipaji
cha kuigiza sauti ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wengine
mbalimbali.
No comments:
Post a Comment