Social Icons

Friday, April 24, 2015

TASWA WAMKUMBUKA BONIFACE WAMBURA

KAMATI ya Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) ilikutana hivi karibuni na kujadili masuala mbalimbali.
 
A ; Katiba ya TASWA
Kamati ya Utendaji ya TASWA imemteua Mwenyekiti wa zamani wa TASWA, Boniface Wambura kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Mabadiliko ya Katiba ya TASWA.
 
Wambura alikuwa Mwenyekiti wa TASWA kuanzia Februari mwaka 2004 hadi Agosti 2010, pia amepata kukaimu nafasi ya Uenyekiti wa TASWA kuanzia mwaka 2003 hadi Uchaguzi Mkuu ulipofanyika mwaka 2004. Kwa sasa Wambura ni Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
 
TASWA inatambua Wambura licha ya kuwa na taaluma ya uandishi wa habari, ni mwanasheria, hivyo inaamini uzoefu wake ndani ya TASWA pamoja na TFF ambako amewahi kuwa Katibu wa Kamati ya Mabadiliko ya Katiba ya shirikisho hilo utasaidia sana kupata katiba nzuri.
 
Wajumbe wengine wa kamati hiyo yenye jumla ya watu watano ni Mhadhiri Msaidizi wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano Kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Egbert Mkoko.
 
Mkoko kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti wa TASWA. Wengine ni Mhariri wa habari za michezo wa gazeti la Daily News, Nasongelya Kilyinga na Mtendaji Mkuu wa Bin Zubeiry Blogspot, Mahmoud Zubeiry, ambaye amepata kuwa Mhariri wa habari za michezo wa magazeti mbalimbali nchini.
 
Mwingine ni mtangazaji wa zamani wa Redio Tumaini Dar es Salaam, ambaye kwa sasa ni mfanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kitengo cha huduma kwa wateja, Domina Rwemanyila. Wajumbe wote ni wanachama wa TASWA.
 
Nia ya TASWA ni kamati hiyo ifanye kazi  ndani ya siku 90 ili Rasimu ya Katiba ijadiliwe katika Mkutano Mkuu wa TASWA unaotarajiwa kufanyika Julai 25 na 26 mwaka huu mkoani Morogoro.
 
B; Media Day
Kila mwaka TASWA imekuwa ikiandaa tamasha maalum kwa ajili ya wafanyakazi mbalimbali wa vyombo vya habari (Media Day Bonanza), ambapo mwaka jana halikufanyika kutokana na sababu mbalimbali.
 
Mwaka huu TASWA imepanga bonanza hilo lishirikishe wadau 2,000 kutoka vyombo mbalimbali vya habari na tayari kampuni mbili zimejitokeza kutaka kudhamini bonanza hilo, lakini si kwa kiwango ambacho chama kinataka.
 
Kutokana na hali hiyo mazungumzo bado yanaendelea na wadhamini hao wametoa masharti ya kupunguza idadi ya washiriki kutoka 2,000 waliopendekezwa na chama hadi kufikia 500, idadi ambayo kwa uzoefu wetu ni ndogo na kwa kadri watu walivyo na hamu ya kujumuika pamoja inaweza isikate kiu ya wanahabari na italeta malalamiko kwa watakaokosa.
 
Nia ya TASWA ni kuwaweka pamoja waandishi wa habari za afya, siasa, uchumi, michezo, mazingira na nyinginezo pamoja na wafanyakazi wa vyombo mbalimbali kujadili masuala yanayowahusu na kisha kuburudika kwa pamoja.
 
Kutokana na hali hiyo TASWA imekubaliana na wadhamini hao, watafutwe wadhamini wengine waongeze nguvu na kufanya bonanza hilo liwe la aina yake na tuna imani katika wiki chache zijazo suala la Media Day litakuwa limekamilika.
 
Kwa mazingira hayo Kamati ya Utendaji katika kurahisisha jambo hilo, imeunda kamati maalaum ambayo Mwenyekiti wa TASWA FC, Majuto Omary atakuwa ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Media Day na Katibu wake atakuwa Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando.
 
C; Mafunzo
Kama tulivyopatangaza mwezi uliopita, TASWA inaendelea na programu za mafunzo kwa waandishi wa habari za michezo, ambapo awamu ya kwanza ilifanyika Machi 25 mwaka huu na kuhusisha washiriki 40, ambapo 30 walikuwa chipukizi na 10 wa kada ya kati.
Awamu nyingine mbili zinatarajiwa kufanyika mwezi ujao, ambapo awamu ya kwanza itakuwa Dar es Salaam mapema mwezi ujao ikihusisha washiriki 40 kati yao 30 ni wa kada ya kati na 10 wakiwa waandishi wazoefu. Awamu ya pili itafanyika mwishoni mwa mwezi huo.
 
Nawasilisha,
 
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
22/04/2015
0717-665544
 

No comments:

 
 
Blogger Templates