Social Icons

Saturday, April 18, 2015

BASATA YAWASHANGAA MISS TANZANIA KUKURUPUKA

 KATIBU Mkuu wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) Godfrey Mngereza.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino International Hashim Lundenga  ambao ndiyo waandaaji wa shindano la Miss Tanzania

BARAZA la Sanaa la Taifa (Basata), limeushangaa uongozi wa Kampuni ya Lino International Agency ambao ni waandaaji wa shindano la Miss Tanzania, kukurupuka na kwenda kukata rufaa kupinga kufungiwa kwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni Michezo na Utamaduni, kwani wangeweza kubaki barazani na kuzungumza nao.

Baraza hilo lilisimamisha shindano hilo kwa miaka miwili kutokana na waandaaji kukiuka kanuni, ikiwamo mawakala kutokuwa na vibali kutoka Basata, kabla ya wahusika kuamua kuandika barua kwa Waziri mwenye dhamana na michezo, Dk. Fenella Mukangara, kupinga adhabu hiyo.

Akizungumza  Ofisini kwake Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam juzi, Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza, alisema Kamati ya Miss Tanzania chini ya Kampuni ya Lino International Agency, inatakiwa kujipanga upya katika kuandaa shindano lenye ubora ili watakapotoka kifungoni waje na sura mpya kutokana na kushuka kiwango siku baada ya siku.
Alisema Miss Tanzania walipaswa kukaa na waandaaji wao na kuwaeleza kilichotokea, halafu wangechanganya mawazo kwa kushauriana, kwani penye wengi pana mengi.
“Baada ya Basata kutoa tamko la kuwataka Lino wajipange na kuweka sawa changamoto zilizojitokeza ambazo wao wanazijua kwa undani zaidi...Tulitegemea Kamati ya Miss Tanzania ingekutana na wadau wake ikiwa ni pamoja na wakala wake wa mikoa kadhaa kama siyo wote, ambao wangewawakilisha wengine ili waweze kuchanganua na kutafakari adhabu waliyopewa, kwa sababu suala hili siyo la mtu mmoja mmoja,” alisema Mngereza na kuongeza.
Tunatambua kwamba shindano hili la urembo nchini lina mashabiki wengi, pia huzalisha ajira nyingi, kwa sababu hata hao warembo wenyewe ambao ndiyo huwa washiriki nao wako pale kwa sababu ya kupata riziki ambayo hutolewa na waandaaji kama zawadi na kifuta jasho...Pia ajira zingine hupatikana kwa wenye kumbi, wasanii, wenye vyombo vya miziki, wauza vinywaji na hata wakaanga chipsi nao huo huwa ni msimu wao, lakini wote tunapaswa kufuata taratibu.
Alibainisha kuwa, hitaji kubwa la Basata kutoka Miss Tanzania ni kuona mfumo wa uandaaji na muendeshaji umebalilika, kamati inaundwa kwa kuzingatia jinsia hasa wanawake, ambako hivi sasa hilo halipo.
“Waandaaji wangekuja na mkakati mpya wa kuandaa shindano hilo, tungekaa mezani  na kushauriana nini kifanyike, wapi wamekwama ili shindano lirudi katika hadhi yake...Ni ukweli lilishuka hivyo tunaamini kwamba hili jambo endapo likitiliwa mkazo basi Miss Tanzania watarudi katika hadhi yao.
“Lino wajipange na kutatua changamoto na kuboresha mfumo mzima wa uandaaji, hasa zile wanazozifahamu kwani hata jamii inazijua baadhi ya changamoto hizo, ikizingatiwa hivi sasa tuko nje ya wakati wa uandaaji, nasisitiza waje na mpango mpya ambao utaonyesha matumaini na imani yetu ni kwamba wataleta, japo hadi hivi sasa hawajaleta mpango wowote mpya,” alisema Mngereza.
Pia, ameitaka kamati iweke wazi mikataba yake na warembo, wazazi wa warembo washiriki wanapaswa kushirikishwa na kuridhia, hivyo wajipange zaidi kuliko kukaa na kumtafuta mchawi, shindano ni lao na halitapewa mtu mwingine ama taasisi nyingine kuratibu.
“Sisi Basata tumefuata ‘process’ zote, hivyo hakuna suala la kufungulia shindano kwa masharti mapya, kwani hata mimi nilisoma kwenye vyombo tofauti vya habari kwamba Basata imefungulia shindano la Miss Tanzania, hatuwezi kuwafungulia kimya kimya...Jinsi tulivyowasimamisha kwa barua na kutangaza kwenye vyombo vya habari, ndivyo hivyo hivyo tutakavyo wafungulia,” alisema.

Aidha, amewataka Miss Tanzania wasionge hatua iliyochukuliwa na Basata kuwa ni uonevu kwao, bali wachukulie kama ni kipindi cha wao kujipanga vizuri zaidi kwa program yao huku akiwataka wadhamini wawe na imani na shindano hilo kwa ujumla.
Chanzo cha shindano hilo kufungiwa ni baada ya kuibuka kwa madai kuwa mshindi taji hilo, Sitti Mtemvu, kadanganya umri wake pia kamati ikashindwa kuthibitisha umri sahihi, jambo ambalo likafanya Basata wakaamua kulichimba zaidi shindano hilo na mwisho wakatoka na uamuzi wa kulifungia shindano kwa miaka miwili na kuwataka wajipange upya.

No comments:

 
 
Blogger Templates