Social Icons

Monday, April 27, 2015

ALLY CHOKI AFUNIKA UTAMBULISHO WA TWANGA


 Wanenguaji wa bendi ya Twanga Pepeta waksaidiana kufungua begi alilokuwemo mnenguaji Hassan Mussa 'Super  Nyamwela' (PICHA ZOTE NA MICHAEL MACHELA)
 Small Nyamwela akitoa shoo mara baada ya kupanda  jukwaani.
 Choki akipungia mashabiki.
 Kalala Junior  wakwanza kushoto  Choki katikati na Luizer

 Luizer akipungia  mashabiki  hawapo pichani.
 Choki na Luizer wakiimba jukwaani
 Rapa na muimbaji Kabatano wakiimba pamoja katika onyesho hilo.
 Safu ya wanenguaji wa kike wa bendi ya Twanga Pepeta.
 Choki akienda sambamba katika kucheza  na wanenguaji wa kiume
 Wanenguaji wa bendi ya Twanga Pepeta wakiongozwa na Lilian Tungaraza 'Internet' wakinengua na Mtangazaji Isack Gamba  huku akiwatunza.

DAR ES ASALAAM

“WALIMWENGU wabaya walimtesa Chokii..” hivyo ni vionjo alivyoingia navyo mwanamuziki nguli, Kamarade Ally Choki kwenye onyesho la kumtambulisha lililofanyika kwenye ukumbi wa Mango Garden Kinondoni jijini Dar es Salaam, juzi usiku.

Baada ya kibwagizo hicho, wapiga vyombo wakazima, kisha Choki akaimba kibwagizo cha wimbo wake mpya, kilichosema ‘Usiyempenda kaja... usiyempenda karudi chungulia umuone,’ huku akicheza kwa staili mpya ya kuweka mkono juu ya macho na kubonyea kidogo kama anachungulia.

Choki na wanamuziki wengine wa Twanga, waliimba na kucheza sambamba huku wakiwaduwaza mashabiki jinsi walivyoonyesha umahiri wao.

Kamarade Choki, ambaye mashabiki walimsubiri kwa hamu kumwona katika jukwaa la Twanga Pepeta baada ya kurejea, alishangiliwa kutokana na namna alivyoingia kwa kibwagizo hicho ambacho kinapatikana katika wimbo wake mpya wa ‘Kichwa Chini’ ambao ni wimbo wake wa 13 ndani ya Twanga.

Licha ya kuwa wimbo huo ulikuwa ni mpya katika masikio ya mashabiki, lakini ghafla kila mmoja aliyekuwepo aliweza kuimba kibwagizo hicho kilichoonekana kukamata ghafla mara baada ya wimbo huo kuimbwa na kuomba urudiwe zaidi ya mara mbili.

Choki alipanda jukwaani saa sita na nusu usiku huku akiunganisha ngoma zake zote ambazo ziliwakuna ipasavyo mashabiki wengi waliojitokeza.

Licha ya kuwa na tishio la mvua na manyunyu ya hapa na pale, lakini mashabiki walianza kuingia ukumbini kuanzia saa moja jioni na hata ilipotimu saa tatu hadi saa nne watazamaji walioingia walipata usumbufu wa kutafuta mahali pa kukaa.

Mwanamuziki huyo mwenye mvuto na mashabiki lukuki, alijitangaza kuwa hivi sasa anafahamika kwa jina la Sir. Cho, jina ambalo alipewa alipokuwa nchini Japan.

Baada ya kuimba wimbo huo mpya, pia Choki aliimba nyimbo kadhaa alizoimba miaka ya nyuma kama ‘Password’, ‘Chuki Binafsi’ na nyinginezo, ambako muda wote mashabiki walionekana kupagawa na kwenda kumtuza.

Akiwa jukwaani, Choki alisema anawashukuru mashabiki na kuwaomba wajipigie makofi kwa kuja katika shoo ya utambulisho wake.

Katika onyesho hilo, pia mnenguaji mahiri, Hassan Mussa ‘Super Nyamwela’ alitambulishwa, ambaye aliingia kwa mtindo wa kubebwa katika sanduku la nguo.

Akiwa ndani ya sanduku hilo, wanenguaji wenzake waliliburuza kwa matairi na kumpandisha jukwaani bila ya watazamaji kutambua nini kilikuwa kikiendelea na mara baada ya kulifikisha, wakasema wanatoa zawadi ndipo Super K alipovuta zipu huku ndani akiwemo Nyamwela na kushangiliwa na mashabiki.

Naye Kiongozi Mkuu wa bendi hiyo, Luizer Mbutu, alitangaza nafasi za Choki ndani ya bendi hiyo kuwa ni Mkuu wa nidhamu, Kiongozi Mkuu Mtendaji na Mkuu wa steji.

No comments:

 
 
Blogger Templates