Social Icons

Friday, February 27, 2015

TWANGA PEPETA NA FM ACADEMIA WAPANIANA FEBRUAARI 28


RAIS wa bendi ya FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’, Nyoshi El Saadat, ametamba kwamba pambano lao na African Stars ‘Twanga Pepeta’ litakalofanyika viunga vya ufukwe wa Escape One Mikocheni Dar es Salaam Machi 28 mwaka huu, litaandika historia katika tasnia ya muziki wa dansi na hata kwa bendi hizo mbili nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Nyoshi alisema Ngwasuma wako vizuri hivyo wapinzani wao wanapaswa kujipanga vilivyo.

“Mimi nawambia bendi ya Twanga Pepeta wajiandae kupambana na sisi kuanzia mavazi hadi kuwajibika jukwaani, kwa sababu bendi ya FM Academia imesheheni wanamuziki wenye sifa na wanaoujua muziki wa dansi,” alisema Nyoshi na kuongeza.

Bendi ya Twanga Pepeta na mashabiki wake, wajitayarishe kuona viuno vikinengua katika kiwango cha hali ya juu kutoka kwa wanenguaji wa Ngwasuma.

Naye Kiongozi wa Twanga Pepeta, Luizer Mbutu, alijibu mapigo kwamba, siku hiyo wataanza na Nyoshi kwa kumfundisha namna ya kuimba katika lugha ya Kiswahili fasaha.

“Twanga tutawaonyesha kazi FM kwamba sisi tunaujua muziki, hivyo siku hiyo lazima wakae na waamuzi watakuwa mashabiki wenyewe,” alisema Luizer.

Alisema wana safu iliyokamilika, hivyo mashabiki watarajie kuona wachezaa shoo ambao wataonyesha umahiri wa hali ya juu pamoja na sebene la nguvu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Twanga Pepeta, Asha Baraka, aliongeza kuwa maandalizi ya pambano hilo ambalo wana imani kubwa litakuwa la aina yake na kuandika historia kwenye muziki wa dansi nchini, yanaendelea vizuri chini ya udhamini wa Clouds Media Group, ambao ndio waliojitokeza kwa sasa.

No comments:

 
 
Blogger Templates