Social Icons

Wednesday, September 17, 2014

SIKINDE NGOMA YA UKAE KUZINDUA ALBAM YAO OKTOBA


BENDI kongwe ya muziki wa dansi nchini, Mlimani Park 'Sikinde Ngoma ya Ukae' inatarajia kuzindua albamu  yake mpya ya 'Jinamizi la Talaka' mwishoni mwa Oktoba baada ya kushindwa kufanya hivyo  mwezi uliopita.

Baada ya uzinduzi huo bendi hiyo inatarajiwa kufanya ziara ya kimuziki katika mikoa ya Morogoro na Dodoma  kwa ajili ya kuzitambulisha nyimbo zao mpya za albamu hiyo kwa mashabiki wa mikoa  hiyo.

Msemaji Msaidizi wa Sikinde, Emmanuel Ndege alisema jana jijini Dar es Salaam  kuwa baada ya kukwama  kufanya uzinduzi wao Agosti kama ilivyokuwa imetangazwa, Sikinde sasa inatarajiwa kuzindua  albamu yao mpya katika maadhimisho ya miaka 38 ya kuanzishwa kwa bendi hiyo.

Ndege alisema kwa sasa wanaendelea kufanya mchakato wa wadhamini kabla ya kutangaza rasmi  tarehe ya jambo hilo, japo alisisitiza itakuwa mwishoni mwa Oktoba.

"Uzinduzi wa albamu yetu mpya utafanyika Oktoba sambamba na maadhimisho ya miaka 38  tangu kuanzishwa kwa Sikinde," alisema Ndege.

Pia aligusia juu ya ziara ya kimuziki wanaotarajia kuifanya wiki ijayo katika mikoa ya Morogoro na  Dodoma ili kutambulisha nyimbo zao mpya kwa mashabiki wa bendi hiyo wa mikoa husika.

"Tupo katika maandalizi ya kwenda kuzitambulisha nyimbo za albamu yetu mpya katika mikoa ya  Dodoma na Morogoro, tukiwa huko pia tutakumbushia nyimbo za zamani za bendi hiyo zilizoipa  Ubingwa wa Muziki wa Dansi Tanzania," alisema Ndege .

No comments:

 
 
Blogger Templates