Social Icons

Wednesday, December 5, 2012

UNCLE D KUZIBA PENGO LA UNCLE JJ BONGO MOVIE?



Uncle JJ (kushoto) na Uncle D anayejaribu kuvaa viatu vyake
Uncle D
BADO mashabiki wa filamu nchini wanaendelea kuumizwa na kifo cha aliyekuwa nyota wa fani hiyo, Steven Kanumba 'Uncle JJ' ama lile maarufu la 'The Great Pioneer' aliyefariki ghafla Aprili mwaka huu.
 
Tangu alipofariki dunia, mashabiki wake wamekuwa wakisikilizia na kutaka kuona nani atakayeweza kuvaa viatu vya mkali huyo aliyekuwa na kiu kubwa ya maendeleo katika fani yake tangu alipokuwa Kaole Sanaa.
 
Wengi wamekuwa wakijiuliza ni msanii gani atakayeweza kuwaburudisha kwa kiwango alichokuwa akikifanya Kanumba hasa kupitia filamu zake mchanganyiko zikiwemo za kiutu uzima, watoto, kidini na masuala mengi ya kijamii.
 
Japo wapo wasanii kibao waliowahi kufanya kazi pamoja na Kanumba wamekuwa wakiaminiwa huenda wakasimama na kuziba pengo hilo la msanii huyo, hata hivyo hali inaonekana kuwa ngumu.
Hii inatokana na ukweli kwamba marehemu Kanumba, aliiteka mioyo ya mashabiki wengi kiasi imekuwa vigumu kwa mashabiki hao kuruhusu mioyo hiyo kutoa nafasi kwa mtu mwingine kuingia.
Ndio maana hata soko la filamu lilionekana kuyumba tangu Kanumba alipofariki kwa kazi za watu wengine kusahauliwa kwa muda na kukimbiliwa kazi za nyuma za mkali huyo, ingawa kwa sasa hali inaendelea kubadilika kwa watu kuzoea hali halisi iliyotokea.
 
Hata hivyo, huenda mashabiki wa filamu wakasuuzwa roho zao, baada ya Jacklyne Wolper kuamua kutengeneza filamu mpya iitwayo 'After Death' ambayo imemshirikisha msanii asiye na jina, lakini aliyeshabihiana na marehemu Kanumba.
 
Msanii huyo si mwingine bali ni Philemon Latwaza ambaye ndani ya filamu hiyo mpya atafahamika kwa jina la 'Uncle D'.
 
Uncle D, ameigiza na 'watoto wa Kanumba', Jennifer na Patrick, walioibuliwa na filamu za 'Uncle JJ' na 'This is It', sambamba na waigizaji wengine wenye majina waliowahi kucheza pamoja na marehemu Kanumba enzi za uhai wake.
 
Muongozaji wa filamu hiyo, Leah Richard Mwendamseke 'Lamata' alisema ujio wa Uncle D unaweza kuziba pengo la Kanumba kwa kiasi fulani na pengine kuwarudisha mashabiki wa marehemu huko katika 'sononi' mpya ya kumkumbuka.
 
Lamata, alisema wamefyatua filamu hiyo kama njia ya kumuenzi Kanumba na pia kuendelezaa juhudi zake za kuibua na kukuza vipaji vya akina Jennier na Patrick.
 
"Nadhani After Death, itawakumbusha mbali mashabiki wa filamu kwa namna Uncle D alivyomudu kumuigiza Kanumba na hasa kutokana na kufanana naye kwa sura kwa kiasi kikubwa," alisema.
Mbali na Uncle D na watoto Jennifer na Patrick katika filamu hiyo pia wameigiza akina Mainda, Mayasa Mrisho, Ben Blanco, Wolper mwenyewe, Irene Paul, Shamsa Ford na Patcho Mwamba.
Swali la kujiuliza je, Uncle D atamudu kuvaa viatu vya Kanumba kama Lamata anavyodai? Ni suala la kusubiri kuona mara filamu hiyo itakapoachiwa mtaani.

No comments:

 
 
Blogger Templates