Social Icons

Friday, October 22, 2010

KWELI MAPENZI YANAUA

Wivu wa mapenzi umemsababishia ulemavu wa maisha dada huyu mkazi wa kijiji cha Izia, Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, aliyetambulika kwa jina la Grace Senga (29) baada ya kung’atwa ulimi na kipande kutolewa wakati wakigombea bwana.

Mama yake mzazi aliyetambuliwa kwa jina la Salome Kapele ambaye pia ni Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Izia alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 5 usiku wakati binti yake huyo akitoka kupata mbili tatu katika klabu ya pombe za kienyeji (yaani kunywa pombe ya kienyeji au unaweza sema mataputapu).

Mama huyo alisema kuwa akiwa amelala aligongewa mlango wa wasamaria wema wakimjulisha juu ya tukio hilo la kuvamiwa kwa binti yake huyo japo hakuweza kutoka nje kwa kuhofia usalama wake.

“Siku ya tukio kuna vijana walikuja kunigongea mlango wangu na kunieleza kuwa mtoto wangu anapigwa ila sikuweza kutoka kwani niliogopa iwapo ningetoka……baada ya hapo alikuja kijana mwingine na kunieleza kuwa mtoto wangu amekatwa ulimi baada ya kung’atwa ulimi lakini miye sikuweza kutoka hadi alipokuja mume wake ndipo nilipotoka na kwenda kumkuta akiwa hoi”.

Habari zaidi zinasema kuwa mama yake alikwenda katika eneo alipokuwa akipewa kipondo na kuokota kipande cha ulimi lakini kilikuwa tayari kimevimba na kujaa mchanga.

Binti huyo kwa sasa amelazwa kwenye Hospitali ya Mkowa Rukwa akiendelea kupatiwa matibabu.

1 comment:

Unknown said...

Ni kweli mapenzi yanaua ila zaidi ni sisi wanawake tunapokuwa hatujithamini. Kwani wanaume wana nini zaidi kuliko sisi? Wamezoea kutudharau na sisi tunakubaliana na matendo yao. Mwanaume akiwa na mpenzi zaidi ya mmoja inaonyesha ni jinsi gani alivyodumaa kiakili na kutopanuka kimawazo. Huyu dada yetu Grace Senga, naamini alikuwa anajua kabisa kuhusu mwanamke mwingine. Angemuacha mapema yote haya yangetokea? Tusiwalaumu wanaume peke yao, sisi wanawake pia tunachangia. Haipendezi mwanadada mpaka saa tano usiku upo kilabuni!! Kama unapenda pombe nenda kanunue mapema unywe nyumbani, yote haya yasingekukuta. Ukiona mwanaume ana manga manga achana nae. Tukijithamini na kujiheshimu ndugu zangu yote haya hayawezi kutukuta. Sasa hasara ya nani? Mpenzi wako sasa yupo safi anajichanganya na kidada wengine. Hebu ona ulivyompa aibu mama yako ambaye ni mtu muhimu hapo mtaani. Tufikirie mbele kabla ya maamuzi. S.K.

 
 
Blogger Templates